WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imewaagiza wamiliki wote wa shule za msingi kusitisha huduma za bweni kwa wanafunzi kuanzia shule ya awali hadi hadi darasa la nne ifikapo mwishoni mwa muhula wa kwanza wa masomo mwaka huu.
Hatua hiyo inatokana na Waraka Namba 2 wa mwaka 2023 uliotolewa Februari 28, 2023 na Kamishna wa Elimu Dk Lyabwene Mtahabwa, ukieleza kuwa shule yoyote itakayotaka kutoa huduma za bweni kwa wanafunzi wa awali mpaka dasara la nne watatakiwa kuandika barua maalum ya maombi.
“Hairuhusiwi kutoa huduma ya bweni kwa wanafunzi wa elimu ya awali na darasa la kwanza hadi la nne isipokuwa kwa kibali maalum kitakachotolewa na Kamishna wa Elimu baada ya kupokea maombi rasmi kutoka kwa mdau husika,” amesema Dk Mtahabwa na kwamba waraka huo unaanza kutumika Machi mosi mwaka huu.
Kwa mujibu wa Kamishna huyo, maagizo hayo ni utekelezaji wa mwongozo wa uanzishaji na usajili wa shule uliotolewa na wizara mwezi Novemba mwaka 2020 na hivyo kuzitaka shule zote zinazotoa huduma ya bweni kwa madarasa yasiyoruhusiwa kusitisha huduma hiyo ifikapo mwisho wa muhula wa kwanza mwaka 2023.
Pia serikali imepiga marufuku shule zote za msingi kuwa na makambi ya kitaaluma na badala yake kuweka mikakati thabiti ya ufundishaji kwa kuzingatia kalenda za mihula, ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.