Serikali yataka muafaka wa GGML juu ya maeneo jirani

SERIKALI kupitia Wizara ya Madini imeuagiza Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) kuandaa na kuwasilisha mpango kazi utakaotatua malalamiko ya majirani wa mgodi waliozuiwa kuendeleza maeneo yao bila fidia.

Waziri mwenye dhamana, Dk Dotto Biteko alitoa maagizo hayo Desemba 12 baada ya kikao na ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Geita mjini na kuwataka GGML kukamilisha maelekezo ifikapo Januari 9, 2023.

Amesema taarifa ya GGML iliyowasilishwa kwenye majadiliano ya mahitaji ya aridhi iliyo ndani ya leseni ya mgodi imeshindwa kujibu changamoto ambazo zilipaswa zipatiwe majibu kutokana na malalamiko ya wananchi.

“Baada ya hapo tutatoa mwelekeo maalumu juu ya hatima ya jambo hili, ni imani yetu ni kwamba kama ilivyo dhamira ya Mheshimiwa Rais, jambo hili liishe na wananchi washughulike na mambo mengine siyo jambo hili kila siku.

“Kuna watu wanaokaa ndani ya vigigingi maisha yao yote wameambiwa wasiendeleze chochote, tujue wanalipwa fidia au wanaachiwa maeneo yao.” Amesema Dk Biteko.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella ameipongeza Wizara ya Madini kwa kutafuta suluhu ya kudumu juu ya changamoto hiyo kulenga kumaliza kilio hicho cha muda mrefu kwa wananchi ambao ni majirani wa GGML.

Mbunge wa Geita Mjini, Costantine Kanyasu amewaomba wananchi wanaomiliki ama kukalia maeneo yanayozunguka mgodi wa GGML kuwa watulivu kwani tayari kilio chao kinaendelea kusikilizwa kupata suluhisho.

Makamu wa Rais wa Mgodi wa GGML, Simon Shayo amesema wapo tayari kushirikiana na ofisi ya mbunge, mkuu wa mkoa pamoja na tume maalumu iliyoundwa kushughulikia tatizo hilo ili kufikia suluhu ya kudumu.

“Lengo likiwa ni kufikia wakati huo ambapo mheshimiwa waziri ametoa basi tuweze kumaliza na pengine kuwe na mapendekezo yanayoangalia mahali ambapo tunaweza kuangalia haki ya kila mtu na wajibu wetu sisi.” Amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button