Serikali yatenga bil 12/- Tazara kuongeza ufanisi

SERIKALI imesema kwa mwaka wa fedha 2022/2023 imetenga zaidi ya Sh bilioni 12 kwa ajili ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) ili kuongeza ufanisi katika usafirishaji wa abiria na mizigo ya ndani na nje ya nchi hususani inayopitia Bandari ya Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete jijini Mbeya baada ya kutembelea stesheni, karakana na Mgodi wa uzalishaji kokoto wa Kongolo.
Mwakibete amesema Tazara imekuwa ikisafirisha mzigo wa Zambia, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na ili kuongeza idadi ya mzigo, serikali imeendelea kutenga fedha kila mwaka ili kuhakikisha mzigo unawafikia walaji kwa wakati kupitia miundombinu bora.
“Nchi jirani zinazotuzunguka zinatumia sana reli hii, na wateja hawa ni muhimu sana kuendelea kuwashawishi kutumia reli hii kupitia miundombinu mizuri na tusisahau biashara ni ushindani hivyo lazima tuliweke hili la maboresho kama kipaumbele,” alisema Mwakibete.
Alisema pamoja na uwekezaji mkubwa unaofanywa, aliitaka Tazara kufanya ukarabati wa mara kwa mara wa stesheni zao nchini ili kupunguza changamoto zilizopo ikiwamo upungufu wa viti vya kukalia kwa abiria.
Aidha, alisema ili Mgodi wa Kongolo ujiendeshe kwa faida ni wakati mwafaka kwa Tazara kuwa na mpango madhubuti wa biashara ili kutumia vifaa vinavyonunuliwa kwa tija.
Mbunge wa Kyela na Katibu wa Wabunge wa Mkoa wa Mbeya, Ally Jumbe aliipongeza Tazara kwa kufanya ukarabati wa mara kwa mara wa njia zake na kuhakikisha kuwa treni zinakuwepo na kuondoka kwa wakati.
Naye Meneja wa Tazara Mkoa wa Tanzania, Fuad Abdalla alisema miongoni mwa mikakati inayoendelea kuchukuliwa ili kuongeza ufanisi na kuongeza pato ni pamoja na mamlaka kuingia makubaliano maalumu na kampuni binafsi ikiwamo Kampuni ya Calabash ili kuhakikisha reli hiyo inatumika wakati wote.
Fuad alisema Tazara pamoja na changamoto za uchache wa vichwa vya treni na behewa, imeendelea kutumia vizuri miundombinu iliyopo kwa kutoa huduma za viwango kwa kusafirisha abiria na mizigo kwa wakati.