Serikali yatoa maelekezo Skimu ya Lyamaigwa

DODOMA; SERIKALI imetoa maelekezo kuhusu ucheleweshaji wa ujenzi wa Skimu ya Lyamaigwa iliyopo jimbo la Bukene, mkoani Tabora.
Maelekezo hayo yametolewa leo na Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Bukene, Suleiman Zedi aliyehoji kuhusu kasi ndogo ya mkandarasi kwenye ujenzi wa skimu ya umwagiliaji ya Lyamalagwa, hivyo kutaka kauli ya serikali kumharakisha mkandarasi huyo, ili wananchi wanufaike kwa kilimo cha mpunga.
“Nimuondoe hofu Mheshimiwa Selemani Zedi, Mbunge wa Bukene, skimu hiyo tayari ina mkandarasi na yuko kazini, lakini bahati mbaya ni kwamba yupo slow. Naielekeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwenda katika eneo hilo kumsukuma huyu mkandarasi, lakini kuona changamoto gani zinamfanya achelewe kufanya hiyo kazi,” amesema Naibu Waziri.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Kalambo, Josephat Kandege, alihoji lini serikali itaanza na kukamilisha ujenzi wa skimu za umwagiliaji katika maeneo yote ya Wilaya ya Kalambo yaliyobainishwa kuwa ni fursa kwa kilimo.
“Katika mwaka 2024/2025 Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini ikiwemo upembuzi yakinifu na usanifu wa skimu za Ilimba, Mkowe, Santamaria, Sopa, Kamawe, Kasanga, Katete, Mtuntumbe, Kasitu, Tatanda, Mao, Katazi, Mnazi, Kaluko, Kilesha, Kambo, Kalembe, Ulumi, na Katuka zenye ukubwa wa jumla ya hekta 21,300 zilizopo katika Wilaya ya Kalambo.
“Upembuzi wa skimu hizo unatarajiwa kukamilika mwaka 2025/2026 na kuanza taratibu za kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi,” amesema Naibu Waziri.