Serikali yazungumzia ushirikiano na sekta binafsi

FISI ya Msajili wa Hazina (OMH) imesema serikali iliamua kushirikiana na sekta binafsi katika uendeshaji wa baadhi ya mashirika ili kuongeza ufanisi, mtaji na matumizi ya teknolojia katika kuendeleza uchumi wa nchi.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji, Ufuatiliaji na Tathmini ya Mashirika ya Kibiashara kutoka OMH, Lightness Mauki, amesema kuwa ushirikiano huo ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuimarisha ufanisi wa mashirika pamoja na kuvutia uwekezaji.
Mauki ametoa kauli hiyo leo ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea mkutano wa Wakurugenzi wa Bodi za kampuni ambazo serikali ina hisa chache, unaotarajiwa kufanyika Machi 16 hadi 18 mwaka huu jijini Arusha.
Akifafanua historia ya uamuzi wa serikali kushirikiana na sekta binafsi, alisema miaka ya nyuma serikali ilikuwa na zaidi ya mashirika ya umma 400, lakini baadaye iliamua kuuza baadhi yake kwa sekta binafsi na kubaki na machache ambayo inamiliki hisa chache.
“Yalikuwa zaidi ya mashirika 400. Tuliamua kuuza baadhi kwa sekta binafsi na kubaki na kampuni 56 ambazo tuna hisa chache,” alisema Mauki.
Alisema ushirikiano huo una manufaa kwa pande zote mbili: sekta binafsi inapata fursa ya kuwekeza na kupata faida, huku Serikali ikipata gawio na kuhakikisha uwekezaji unawanufaisha wananchi.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, gawio kutoka kwa kampuni ambazo Serikali ina hisa chache limeongezeka kwa asilimia 357, kutoka Sh bilioni 58.26 mwaka 2020 hadi kufikia Sh bilioni 266.52 mwaka 2024, ikionesha ukuaji mkubwa na mafanikio ya mkakati wa kushirikiana na sekta binafsi.
Mauki Alisema kuwa katika kipindi hicho hicho, uwekezaji wa serikali katika kampuni ambazo inamiliki hisa chache uliongezeka kwa asilimia 140, ukipanda kutoka Sh trilioni 1.5 hadi Sh trilioni 3.6, jambo linaloashiria ukuaji endelevu na ufanisi wa mkakati wa kushirikiana na sekta binafsi.



