SGR kusafirisha mizigo Dar-Dodoma Juni

DODOMA : WAZIRI wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeanza maandalizi ya kusafirisha mizigo kwa kutumia reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, huduma ambayo inatarajiwa kuanza rasmi mwezi Juni mwaka huu.

Profesa Mbarawa alitoa kauli hiyo jana mjini Dodoma wakati akihitimisha mjadala wa bajeti ya Wizara ya Uchukuzi ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/2026 bungeni.

Amesema tayari baadhi ya wadau wameanza kualikwa ili kuchangamkia fursa hiyo, ambayo inalenga kuongeza mapato ya serikali kupitia sekta ya usafirishaji.

“Yako makampuni mbalimbali ya Watanzania yaliyoonyesha nia ya kufanya kazi ya uendeshaji wa mizigo kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, hasa kwa kuwa biashara kubwa ipo kwenye mizigo,” alisema Profesa Mbarawa.

SOMA: Mradi wa SGR Isaka – Mwanza wabadilisha maisha ya wananchi

Ameongeza kuwa serikali pia imeanza mchakato wa kufufua usafirishaji wa reli katika ukanda wa Kusini na Kaskazini, maeneo ambayo yana fursa kubwa za kiuchumi.

“Reli ya Kusini ni muhimu sana kwa sababu kuna madini mengi. Naamini tukijenga reli hiyo, uchumi wa maeneo hayo utafunguka kwa kasi,” alisema.

Wakati huo huo, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeidhinisha na kupitisha bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ambapo jumla ya Sh trilioni 7.4 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya miundombinu ya uchukuzi.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button