Sh Bil 34 kuwezesha usafiri kwa wajawazito
TANZANIA itapokea msaada wa Dola Milioni 15 (takribani shilingi Bilioni 34), kutoka Kampuni ya Vodafone, ili kuwezesha usafiri wa dharura kwa wajawazito.
Ahadi hiyo imetolewa katika kikao cha pembezoni cha Mkutano Mkuu wa 77 wa Wakuu wa Nchi (UNGA) unaoendelea jijini New York, Marekani.
Katika kikao hicho, chini ya uenyekiti wa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID), Samantha Power, Mkuu wa Masuala ya Kimataifa wa kampuni ya Vodafone, Joachim Reiter aliwasilisha ahadi ya kampuni hiyo kutoa fedha hizo, ili kutekeleza mradi huo ikiwa ni hatua ya kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kukuza uchumi nchini.
Alieleza kuwa kampuni binafsi zina jukumu muhimu la kushirikiana na serikali kuleta maendeleo na kuchangia ustawi wa jamii.
Serikali ya Marekani kupitia USAID huzipatia pia kampuni binafsi fedha, kuwezesha kufikia nchi zenye uhitaji mkubwa.
Akimwakilisha Rais Samia katika mkutano huo, Makamu wa Rais Dk Philip Mpango, aliishukuru Vodafone.
Dk Mpango alieleza kuwa Tanzania takribani wanawake 4,000 na watoto 65,000, hufariki kila mwaka, huku kuchelewa kupata huduma za dharura ikiwa ni pamoja na usafiri wa dharura kukichangia sehemu ya vifo hivyo.
Naye Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, aliyeambatana na Makamu wa Rais katika mkutano huo, alieleza furaha yake kwa Tanzania kupatiwa mradi huo na kwamba utaisaidia kufikia malengo iliyojiwekea katika mkakati wa tano wa afya na Mpango Mkakati wa Tatu wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, ambayo moja ya vipaumbele ni kupunguza vifo vya wajawazito na watoto.