SERIKALI imetenga jumla ya Sh bilioni 55.9 kwa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kwa ajili ya kuboresha huduma za tiba na shughuli za uendeshaji.
Hayo yameelezwa leo Agosti 3, 2023 na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya MOI, Prof. Abel Makubi wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Majukumu ya Taasisi hiyo ndani ya miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Sita na Mipango ya mwaka 2023-2024.
Amesema lengo ni kuongeza ubora wa huduma zote za ndani, ili kukidhi matarajio ya wananchi na kufikia viwango vya kimataifa.
Amesema taasisi hiyo imeanzisha huduma mpya tatu za kibingwa bobezi, ambazo zinapunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi kusaka matibabu.
Ametaja matibabu hayo ya kibingwa ni tiba ya baadhi ya kiharusi kupitia angio-suite, tiba ya baadhi ya vifafa kupitia upasuaji na upasuaji wa kiuno kwa njia ya matundu (Hip arthroscopy).
Ameeleza mipango mingine ni ukarabati wa miundombinu ya hospitali, ujenzi mpya miundombinu, ujenzi wa jengo jipya la wagonjwa wa nje (OPD), ambalo litakuwa na vyumba 30 vya kliniki vya kisasa tofauti na vyumba saba vilivyopo sasa.
Amesema pia ujenzi wa hospitali ya kisasa ya utengamao, mazoezi ya viungo na upasuaji wa mifupa (Rehabilitation and Spine centre) katika kiwanja cha MOI chenye ukubwa wa hekari 10 kilichopo Mbweni Mpiji jijini Dar es salaam.
“Kuhakikisha vifaa tiba vinapatikana muda wote zimetengwa shilingi Bilioni 2, kwa mwaka huu kupunguza gharama za upasuaji kwa kununua vifaa moja kwa moja kutoka viwandani,” amesema Prof .Makubi.
Amesema MOI inaendelea kuwapa mafunzo wataalamu ili kuwaongezea ujuzi, ambapo wataamu 10 wanapelekwa kwenye mafunzo kupitia mfuko wa mafunzo wa Mama Samia.
Amesema MOI inaendelea pia kujengea uwezo watumishi wa hospitali zingine za Kanda na Mikoa, ili kupunguza mrundikano wa wagonjwa MOI na kutoa nafuu ya gharama kwa wananchi.
“Kutoa elimu kwa kushirikiana na mamlaka nyingine ili kupunguza ajali za barabarani na kukabiliana na majanga,” amesema.