Sh bilioni 1 kuboresha soko Manzese
KIASI cha Sh bilioni 1.3 zimetengwa na Manispaa ya Ubungo mkoani Dar es Salaam, kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa uboreshaji wa soko la Manzese maarufu soko la kuku.
Ofisa Mfawidhi sehemu ya biashara na masoko katika manispaa hiyo,, Geofrey Mbwama amesema fedha hizo zimetengwa kutoka mapato yake ya ndani.
Amesema katika uboreshaji huo manispaa hiyo imepanga kujenga fremu za kisasa kwenye ghorofa ya sakafu tatu ambapo jumla ya fremu 39 zitajengwa.
Amesema manispaa imedhamiria kujenga fremu za kisasa kwa wafanyabiashara wa soko hilo hususani wauza kuku ili kuwawezesha kufanya biashara zao kwenye maeneo rafiki yatakayovutia wateja wao na hivyo kuweza kukuza vipato vyao.
Mbwama ametoa rai kwa wafanyabiashara hao kuanza kufanya biashara zao kisasa hususani wafanyabiashara wa kuku ambapo miundombinu itakayokuwepo itawalazimu kutunza kuku kwenye majokofu baada ya kuchinja.
Amesema uboreshaji wa soko unaenda sambamba na sheria ya upangaji miji kwa kuweka miundombinu ya kisasa ikizingatiwa Manzese ni “smart area” na pia ni katikati ya mji.
Pia amesema ni moja ya mkakati wa manispaa wa kubuni vyanzo vipya vya mapato ya ndani ili kuiwezesha kukusanya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ya sekta za elimu, afya na uboreshaji wa masoko.
Naye mfanyabiashara katika soko hilo, Mualami Muya mfanyabiashara wa soko hilo amesema uboreshaji wa soko hilo utasaidia wafanyabiashara kuwa na eneo salama la kufanya biashara zao tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Amesema uwepo wa miundombinu ya kisasa katika soko hilo, utaondoa hasara kwa wafanyabiashara pale ambapo kuku watahitajika kuhifadhiwa kwenye majokofu kwani hali ya sasa inawalazima kulipia kiasi cha fedha ili kuhifadhi kuku wao na wakati mwengine kuku hao upotea.
“Kuna muda mfanyabiashara anapata kuku kutoka mikoani hadi wakifika mjini kuku hao wanachoka sana na ndipo itamlazimu muuzaji kuchinja kuku hao na kuwahifadhi kwenye majokofu ambayo kwa sasa tunalipia na bado mara zingine muuzaji anaweza kupoteza kuku hao kwenye majokofu hayo,” amesema.
Soko la Manzese Lina jumla ya wafanyabiashara 496 ambapo kati ya hao wafanyabiashara wanaouza kuku ni zaidi ya 100 huku wanaobaki wanajishughulisha na biashara za mama lishe na biashara mchanganyiko.
Pia soko la Manzese ni miungoni mwa masoko 13 ya Manispaa ya Ubungo ambalo pia ni miongoni mwa masoko manne yanayoboreshwa na Manispaa hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 likiwemo soko la Mabibo, soko la Simu 2000 na soko la Mbezi.