Sh bilioni 117 zatengwa miradi Ziwa Victoria, Nyasa,Tanganyika

SERIKALI  imetenga Sh bilioni 117, mwaka wa fedha 2023/2024  kwa ajili ya miradi mingi ya ziwa Tanganyika,Victoria na Nyasa,huku fedha nyingi zitaelekezwa ziwa Tanganyika ambako hakuna meli kabisa.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Huduma za Meli Tanzania (MSCL), Eric Hamissi akielezea mafanikio ya miaka miwili ya Rais Samia Suluhu katika kongamano linaloendelea katika ukumbi wa BOT leo Machi 15, 2023 mkoani Mwanza.

Hamis amesema katika Sh bilioni 117 ambazo zimetengwa, Sh bilioni 42 zitabaki Mwanza kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa meli katika ziwa Victoria, ili kuongeza tija ya utoaji huduma za usafiri wa majini kwa watu na mali zao.

Amesema ujenzi wa meli ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu unaendelea vizuri na tayari meli hiyo imefikia hatua ya kushushwa kwenye maji, hatua ambayo ni muhimu katika ujenzi wa meli.

Ameongeza kuwa kwa hivi sasa serikali pia inaendelea na ukarabati wa meli kubwa ya mizigo inayoweza kubeba shehena kubwa ya mizigo katika ziwa Victoria, ambapo serikali imetumia shilingi Bilioni 19 kwa ukarabati huo.

Habari Zifananazo

Back to top button