KIGOMA: SERIKALI imepeleka sh trilioni 11.4 mkoani Kigoma tangu serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan iingie madarakani.
Fedha hizo zimetumika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma,Thobias Andengenye akitoa taarifa ya mkoa kwa Mwenyekiti wa Umoja wa vijana wa CCM na Mjumbe wa kamati kuu ya CCM, Mohamed Kawaida amesema fedha hizo zimetolewa mkoani humo kwa kipindi cha miaka mitatu.
Amesema pamoja na mambo mengine fedha hizo zimetumika kutekeleza miradi ya umeme kiasi cha sh bilioni 534 ikiwemo umeme wa gridi ya Taifa kutoka Nyakanazi shilingi Bilioni 467.3 na uzalishaji wa umeme wa maporomo ya Igamba shilingi 66.7.
Amesema, serikali pia imepeleka mkoani humo kiasi cha sh trillion 7.32 kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa kilometa 506 kutoka Tabora hadi Kigoma na kilometa 242.5 kutoka Uvinza hadi Msongati.
Katika taarifa yake mkuu huyo wa Kigoma amesema serikali imepeleka mkoani humo kiasi cha sh bilioni 7.2 ukarabati wa meli ya MT Sangara, ujenzi wa meli ya abiria na mizigo sh bilioni 138.6, Meli ya Mizigo sh bilioni 146, Kiwanda cha Meli Bilioni 298 na ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Kigoma sh bilioni 40.
Sambamba na hilo amesema kuwa serikali imewekeza kiasi kikubwa kwenye sekta ya afya ikiwemo kutumia sh bilioni 36 ujenzi wa tawi la chuo kikuu cha afya cha Muhimbi (MUHAS), ujenzi, ukarabati na unoreshaji wa miundo mbinu ya afya ya mkoa na kutumia sh bilioni tano kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya rufaa ya kanda.
Kwa upande wa miundo mbinu ya barabara Andengenye amesema kuwa serikali imetoa kiasi cha sh bilioni 371 kwa wakala wa barabara nchini (TARURA) na Wakala wa barabara za mijini na vijijini (TARURA) kiasi cha sh bilioni 47 huku miradi ya maji ikitumia kiasi cha shilingi bilioni 429.
Nae, Mwenyekiti wa Umoja wa vijana wa CCM, Mohamed Kawaida amewataka viongozi wote nchini kutumi nafasi zao kueleza mambo makubwa yaliyofwa na serikali ya Raisi Samia kwa wananchi wake.
Kawaida amesema kuwa viongozi wa chama hata ngazi za mashina na tawi wanapaswa kuzijua taarifa hizo na kuzieleza kwa wananchi kwenye maeneo yao bila kificho wala woga kwani Raisi Samia amefanya kazi kubwa kwenye kipindi kifupi cha utawala wa awamu yake ya sita madarakani kama Raisi wa nchi.