Shirika lapendekeza mahakama mashauri ya ukatili

SHIRIKA la Wanawake katika Sheria barani Afrika (WiLDAF), limependekeza kuwe na mahakama itakayoshughulikia mashauri ya familia zikiwamo kesi za ukatili ili kurahisisha upatikanaji wa haki.

Aidha, limependekeza kuwapo kwa sheria maalumu ya kushughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia ili kusaidia uendeshaji wa mashauri.

Mkurugenzi wa WILDAF, Anna Kulaya alisema hayo Dar es Salaam jana baada ya kuwasilisha mapendekezo zaidi ya 20 mbele ya Tume ya Haki Jinai nchini na akasema mapendekezo yao yamezingatia masuala ya wanawake, watoto na walemavu katika haki jinai.

“Mahakama ya Kituo Jumuishi Temeke yenyewe inahusika na masuala mengi ikiwemo mirathi na ndoa, lakini mahakama tunayoiomba iwe inashughulikia kesi, mfano mtoto amepigwa na mama yake au ukatili wowote wanaofanyiwa ikiwemo kubakwa na kulawitiwa na ndugu wa familia na isichanganywe na vitu vingine kitu ambacho kitasaidia upatikanaji wa haki haraka,” alieleza Kulaya.

Pia alisema kuna ukatili unafanywa na ndugu wa familia au wanandoa wenyewe hivyo tume hiyo ione namna ya kuhakikisha usalama wa wanawake na watoto wanaofanyiwa vitendo hivyo.

“Kuna watoto wanafanyiwa ukatili na ndugu zao, lakini kabla ya kesi kuisha, wanakuwa nyumba moja na washitakiwa hivyo huondoa usalama wake. Ili kuwe na haki jinai kwa watu waliofanyiwa vitendo vya ukatili, wanapaswa kuondolewa nyumbani ili kuwepo na usalama kwa kuwa kesi nyingi zinashindwa kuendelea kwa sababu wadaawa wanaishi nyumba moja hivyo kuongeza vitisho,” alifafanua Kulaya.

Pia wamependekeza kuwe na sheria inayoshughulikia kesi za ukatili wa kijinsia kama ambavyo Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), Sheria ya Kanuni ya Adhabu na Sheria ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu zinazohusika na haki jinai.

Kulaya alisema sheria hizo zinataja mashitaka ya ubakaji, ulawiti na shambulio la aibu kwa pamoja na makosa mengine ambayo hayahusiani na ukatili.

“Tumependekeza iwepo sheria itakayohusu ukatili kwa wanawake, watoto na wenye ulemavu kwani nchi yetu ni mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambayo ina vipengele hivi hivyo ipo haja ya kuwa na sheria hizi,” alieleza.

Kuhusu gharama za uchukuaji vipimo vya vinasaba (DNA), Kulaya alisema WiLDAF imependekeza kuwapo kwa vituo vya kuchunguza masuala ya kisayansi mikoa yote nchini sanjari na kupunguzwa kwa gharama za DNA.

Alisema DNA ni miongoni mwa taarifa za kiuchunguzi zinazohitajika katika kesi za ukatili, na gharama zake kwa kiwango cha juu ni Sh 300,000 ambayo wakati mwingine walalamikaji wakiwamo wanawake hawazimudu.

Pia alisema idadi ya wanawake waliopo magerezani inaongezeka hivyo mifumo iangaliwe kuwe na maeneo ya kuwanyonyesha watoto na pia iwalinde.

Habari Zifananazo

Back to top button