KIKOSI cha Kudhibiti biashara ya magendo kimefanikiwa kukamata tani 13.25 ya shehena za sigara bandia aina ya supermatch zilizoingizwa nchini kutokea nchi jirani ya Burundi kinyume cha sheria.
Meneja Msaidizi wa Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) Forodha mkoani Mwanza, Oswald Massawe amesema hayo leo Januari 21, 2023 walipofika kichomea taka Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) kwa ajili ya kuziteketeza.
Amesema shehena hiyo ilikamatwa katika eneo la Mahundi, katikati ya Isaka na Tinde mkoani Shinyanga Septemba 3, 2022 ikiwa kwenye gari namba T220DCQ na tela namba T897BVF.
“Dereva awali amesema alikuwa amebeba kahawa, aina ya arabika, na alikuwa akiitoa Burundi kuipeleka Kenya, lakini baada ya mahojiano ya kina alikiri kwamba siyo kahawa bali ni sigara.
“Tuliposhirikisha taasisi zingine za serikali wakaenda kuzipima wakagundua kwamba hazifai kwa matumizi ya biandamu, kwa hiyo mara moja walitushauri tuziteketeze.
”
Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga, Faustine Mdessa ameeleza shehena hiyo yenye katoni 2200 kila moja ina sigara 5,000 sawa na jumla vipande vya sigara milioni 11.
Aliwataka wafanyabiashara kuepuka biashara haramu kwani wanaweza kujikuta wakiingiza bidhaa zenye madhara kwa afya ya binadamu, mazingira na kuinyima serikali mapato.