Simba yapewa Wydad, Yanga yakabidhiwa Ahly

AFRIKA KUSINI; Johannesburg. DROO  ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika imepangwa muda huu nchini Afrika Kusini ambapo Simba imepangwa Kundi B na Yanga imepangwa kundi D.

Simba ipo kundi moja na Wydad Casablanca ya Morocco, Asec Mimosas kutoka Ivory Coast na Jwaneng Galaxy ya Botswana,  wakati upande wa Yanga amepangwa na mabingwa watetezi Al Ahly ya Misri, CR Belouizdad ya Algeria na  Medeama ya Ghana.

Timu 16 kati ya 54 kutoka vyama 42 vya soka Afrika zimepenya hatua hiyo ya makundi baada ya kushinda katika mechi za raundi ya pili, Yanga ikifuzu kwa mara nyingine baada ya kupita miaka 25 tangu ilipocheza mara ya kwanza mwaka 1998 michuano hiyo ilipobadilishwa kutoka Klabu Bingwa Afrika kuwa Ligi ya Mabingwa.

Advertisement

Yanga iliwang’oa Al Merrikh ya Sudan huku Simba ikifuzu kwa kanuni ya bao la ugenini dhidi Power Dynamos ya Zambia.

Yanga iliyokuwa Kundi D la Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2016 inakutana tena na Medeama katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu. Katika kundi hilo Yanga na Medeama zilishindwa kusonga mbele baada ya kumaliza katika nafasi mbili za mwisho.

Hii itakuwa ni nafasi nyingine kwa Yanga kulipa kisasi kwa  Medeama ya Ghana kwani mwaka huo katika mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Dar es Salaam Julai 16, 2016 ililazimishwa sare ya bao 1-1.

Katika mchezo wa marudiano uliopigwa Ghana wiki moja baadae ya Julai 26 mwaka huo, Yanga ilishindwa kutamba  ilinyukwa mabao 3-1 na kuvuna pointi moja tu kati ya sita pindi ilipokutana na miamba hiyo.

Kwa upande wa Simba inakutana na mechi ya kisasi baada ya kupangwa kundi moja na  Asec Mimosas ya Ivory Coast, Wydad Cassablac ya Morocco zikiwa zilishawahi kukutana.

Wydad iliyowatoa Simba kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita.

Simba pia imepangwa na Jwaneng Galaxy iliyowatoa katika raundi ya kwanza tu ya Ligi ya Mabingwa msimu wa 2021/2022 kwa faida ya bao la ugenini baada ya kufungana mabao 3-3.

Akizungumza baada ya droo hiyo Kocha wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ anasema; “Kila mmoja wetu anatambua jinsi gani ambavyo tuna michezo mikubwa na migumu mbeleni ila kwangu kama kocha, wachezaji na viongozi tunajua njia bora ya kutimizia malengo yetu ni maandalizi.”

Kwa upande wa  kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amesema  timu yake ipo tayari kukutana na mpinzani yoyote wakati Meneja wat imu hiyo Walter Harrison akisema kuwa makundi wameyaona na amekiri ni kundi gumu.

Katika michuano hiyo Kundi A lina zipo timu za Memelody Sundowns ya Afrika Kusini, Pyramids ya Misri, TP Mazembe ya DR Congo na FC Nouadhibou ya Mauritania.

Kundi C lina timu ya Esperance za Tunisia,  Petro Atletico ya Angola, Al Hilal ya Sudan na Etoile du Sahel.

Mechi za hatua ya makundi zitaanza kuchezwa rasmi kati ya Novemba 24 hadi 26 na zitamalizika Machi mwakani.