Simba yatinga Robo Fainali CAF

ANGOLA; SIMBA ya Dar es Salaam imetinga Robo Fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Bravos do Maquis mchezo uliofanyika usiku huu nchini Angola.

Kutokana na matokeo hayo Simba imefikisha pointi 10 ikishika nafasi ya pili nyuma ya CS Constantine inayoongoza kundi A ikiwa na pointi 12, baada ya leo kuifunga CS Sfaxien mabao 3-0  mchezo uliofanyika nchini Algeria.

Advertisement

Simba imebakisha mchezo mmoja utakaopigwa Jumapili ijayo dhidi ya CS Constantine Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, mchezo utakaokuwa wa kuwania kumaliza nafasi ya kwanza kwenye kundi.

Hata kama Simba ikifungwa mchezo huo, kisha Bravos yenye pointi saba ikashinda mchezo wake wa mwisho dhidi ya CS Sfaxien, bado Simba itakuwa imefuzu kulingana na kanuni za CAF kwa mashindano hayo kama timu zikilingana pointi kinachoangaliwa kwanza ni timu  husika zilipokutana matokeo yalikuwaje. Simba iliifunga Bravos bao 1-0 mchezo wa kwanza Uwanja wa Benjamin Mkapa.