WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene amesema siasa za kisasa ni kutatua changamoto zinazowakabili wananchi na sio kuzungumza maneno matupu huku.
Amewataka wananchi kuwapuuza wale wote wanaokejeli maendeleo yaliyofanywa na Serikali jimboni kwake na nchini kote kwa ujumla.
Simbachawene amesema hayo wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Kibakwe, Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma ambapo amesema Kibakwe ya sasa ni tofauti na ile ya miaka kadhaa iliyopita.
Amesema mfano mwaka 2005 jimbo hilo lilikuwa dhoofu kwenye huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya, maji, umeme pamoja na barabara lakini kwa sasa imekuwa ni tofauti.
“Kibakwe ninayoiona leo inafurahisha sana, tumetekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa vitendo na kwa kiasi kikubwa sana kwani utitiri wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa mnaiona wenyewe,” amesema Simbachawene.
Akizungumzia mradi wa miundombinu ya barabara jimboni humo, Simbachawene amesema Kibakwe ya sasa imefunguka huku akitaja uwepo wa barabara za lami pamoja na utengenezaji wa barabara kila kona katika Jimbo hilo ukiwa unaendelea.
“Leo tumekagua ujenzi wa barabara ambapo mmeshuhudia wenyewe uwekaji wa lami kuelekea Shule ya Sekondari Kibakwe pamoja na kuelekea Kanisa Katoliki ukiwa unaendelea, hizi ndizo siasa za kileo,” amesisitiza.
Ameongeza kuwa taratibu za kumpata Mkandarasi wa ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutokea Mpwapwa hadi Kibakwe unaendelea.
Akizungumzia kuhusu mradi wa ujenzi wa Chuo cha VETA unaoendelea katika Jimbo hilo la Kibakwe utakaogharimu shilingi bilioni 1.6 hadi kukamilika kwake amesema ukikamilika utatatua changamoto ya ajira kwa vijana nchini, hususan katika Jimbo hilo la Kibakwe.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kibakwe, David Chisanza amemuelezea Simbachawene kuwa ni Kiongozi wa mfano ambaye katika kipindi chote cha uongozi ameendelea kuzigusa familia za wana Kibakwe kwa namna tofauti kimaendeleo.