Simbu aiheshimisha Tanzania, Samia ampongeza
RAIS Samia Suluhu Hassan amempongeza mwanariadha, Alphonce Simbu kwa kuiwezesha Tanzania kupata medali ya kwanza ya dhahabu katika Mashindano ya Riadha ya Dunia tangu nchi ipate uhuru.
Amesema ushindi wake umeandika sehemu ya historia ya taifa na kumtaka aendelee kuipeperusha vyema na kuiheshimisha Bendera ya Tanzania.
“Hongera sana Alphonce Simbu kwa Medali ya Dhahabu ya ushindi wa Mbio Ndefu za Mashindano ya Kimataifa ya Riadha ya Tokyo. Ndani ya saa 2:09:48 umeandika sehemu ya historia ya taifa letu,” amesema Samia kupitia akaunti yake ya Instagram.
SOMA: Samia: Geay, Simbu wameliheshimisha taifa
Rais Samia ameongeza: “Kama nilivyokusihi uliposhika nafasi ya pili kwenye Boston Marathon mwezi Aprili mwaka huu, ushindi wako ni matokeo ya nidhamu yako ya hali ya juu na kujituma kwa bidii kwenye kazi. “Umekuwa mfano bora kuhusu nguzo hizo mbili za kazi kwa wanariadha na wanamichezo wenzako, na hata kwa wasio wanamichezo. Endelea kuipeperusha vyema na kuiheshimisha bendera ya taifa letu”.
Wakati huo huo wadau wa michezo nchini wamempongeza mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 33 kwa kumaliza mbio hizo za kimometa 42.195 kwa kutumia saa 2:09:48 akivuka mstari mbele ya raia wa Ujerumani,
Amanal Petros, aliyeambulia medali ya fedha baada ya kushika nafasi ya pili. Simbu aliwahi kupata medali ya shaba katika Mashindano ya Dunia ya Riadha yaliyofanyika London, Uingereza 2017.
Akizungumza na gazeti la HabariLEO baada kumaliza mbio hizo, Simbu amesema kuwa zilikuwa ngumu kwani wanariadha nyota wengi walishiriki.
“Joto lilikuwa kali sana na wanariadha walioshiriki ni wale waliofikia viwango, hivyo mbio zilikuwa kali sana,” alisema.
Mkuu wa Msafara wa timu hiyo ya riadha, Rogat John amesema Simbu ameiheshimisha Tanzania kwa kupata medali hiyo ya dhahabu. “Kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi, wimbo wetu wa taifa utapigwa kwa dhahabu hiyo,” alisema akizungumza na gazeti hilo.
Mwanariadha wa zamani wa mbio za kati, Seleman Nyambui amesema amefurahi kwa Tanzania kupata medali ya dhahabu.
“Sasa bado katika Michezo ya Olimpiki ndiyo hatujawahi kupata medali ya dhahabu, uongozi mpya wa riadha ujitahidi kuendeleza na michezo mingine pia badala ya marathoni tu,” amesema.
Nyambui na Fibert Bayi wamewahi kupata medali katika Michezo ya Olimpiki ya Moscow 1980 walipopata medali za fedha katika mbio za meta 5,000 na 1,500.
Gwiji wa marathoni nchini, Juma Ikangaa alimpongeza Simbu kwa ushindi huo akisema inadhihirisha Tanzania ilivyo na vipaji vingi vya marathoni.
Ameshauri serikali kutoa fungu la maendeleo ya mchezo huo kama ilivyo kwa soka. Kwa upande wake, mshindi wa rekodi ya dunia ya meta 1,500, Bayi amempongeza mwanariadha huyo kwa ushindi.
“Hizo ni juhudi binafsi za mwanariadha, na anajitahidi sana baada ya kushiriki olimpiki nyingi, hatimaye Mungu amemsaidia ameshinda medali ya dhahabu.”
Mtanzania mwingine aliyewahi kutwaa medali ni Christopher Isegwe pia alitwaa medali ya fedha katika Mashindano ya Dunia ya Riadha yaliyofanyika Finland 2005.



