Simiyu kamili maadhimisho Wiki ya Chakula

MKOA wa Simiyu unatarajiwa kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya Wiki ya Chakula Duniani, yanayotarajiwa kufanyika kitaifa mkoani humo kuanzia Oktoba 10, 2022, ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.

Akizungumza na Kamati ya Maandalizi ya maadhimisho hayo ya kitaifa, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahaya Nawanda, alisema yatafanyika katika Viwanja vya Shule ya Sekondari ya Bariadi na yamelenga katika uhamasishaji wa uzalishaji na upatikanaji wa chakula bora na salama kwa kuanzia ngazi ya familia, kata, wilaya, mkoa na Taifa kwa ujumla.

Alisema pia yamelenga kuhamasisha wananchi kuhakikisha  wanapata lishe bora, ili kupunguza udumavu ndani ya familia na jamii, kwa kutoa nafasi kwa wakazi hao kujifunza namna bora za uhifadhi chakula kwa kutumia teknolojia za kisasa.

 “Tumelenga kuhakikisha wananchi wetu wanapata elimu ya uzalishaji bora wa mazao ya chakula na mifugo, kuhakikisha kila mwanakaya anapata lishe bora katika eneo analoishi, ili kupunguza hali ya udumavu kwa watoto na pia kupambana na magonjwa nyemelezi yanayosababishwa na ukosefu wa lishe bora ndani ya familia husika,” alisema Dk Nawanda.

Alisema pia watatoa elimu ya namna bora ya usindikaji wa mazao ya chakula, ili kukabiliana na changamoto za wimbi la njaa linalozikumba sehemu mbalimbali za mkoa huo, hasa wakati wa msimu wa kiangazi.

Dk Nawanda alisema maadhimisho hayo yatakayomalizika Oktoba 16, mwaka huu, pia yatatoa fursa kwa wajasiriamali wadogo wanaojishughulisha na usindikaji wa mazao ya chakula na mbogamboga, kushiriki kuonesha bidhaa zao na pia kutoa fursa kwa wananchi kujifunza namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Habari Zifananazo

Back to top button