RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema serikali imeamua kuongeza idadi ya barabara zitakazojengwa kwa kiwango cha lami hadi kufikia kilometa 300 mijini na vijijini.
Dk Mwinyi ametoa tamko hilo alipoifungua Barabara ya Ukutini – Bandarini katika Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba jana.
Alisema umuazi huo umefikiwa na serikali baada ya kuongezeka kwa maombi ya wananchi kujengewa barabara katika maeneo mbalimbali.
Alisema serikali imevuka lengo la Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2020/2025 iliyoainisha ujenzi wa kilometa 275 za barabara.
Akizungumzia barabara ya Ukutini – Mtangani bandarini aliyoifungua, alisema ni hatua muhimu ya kufungua fursa za kiuchumi na kuimarisha fursa za kijamii.
“Tutakuwa tumewagusa wananchi kwani barabara ni uchumi,” alisisitiza Dk Mwinyi.
Alisema mbali na usafiri, barabara hiyo itafungua fursa za ajira kwa kuwa kuna bandari na hoteli katika eneo hilo pamoja na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii zikiwamo hospitali, shule na usafirishaji.
Alieleza kuwa mkataba wa wananchi na serikali yao ni Ilani ya Uchaguzi hivyo kuna kila sababu ya kujivunia kwa yote yaliofanyika katika ujenzi wa barabara.
Aliipongeza Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa barabara vijijini na mijini Unguja na Pemba.
Ufunguzi wa barabara hiyo unakamilisha idadi ya kilometa 85.5 za barabara zilizojengwa katika Mkoa wa Kusini Pemba.
Naye Waziri wa Ujenzi, Mawasilaino na Uchukuzi, Dk Khalid Salum Mohammed aliwahakikishia wananchi kuwa serikali haina ubaguzi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo hususani ujenzi wa barabara na zote za Mkoa wa Kusini Pemba zilizomo katika mpango wa ujenzi zitajengwa kwa awamu.
Barabara ya Ukutani – Bandarini yenye kilometa 4.6 iliyojengwa na Kampuni ya IRIS inakisiwa kugharimu Dola za Marekani milioni 2.658, na ni miongoni mwa mradi wa ujenzi wa barabara za ndani zenye urefu wa kilometa 275.9.