SMZ kuongeza uzalishaji wa chakula
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imejipanga kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula ikiwemo mpunga pamoja na mazao ya viungo kwa ajili ya kuiwezesha Zanzibar kujitosheleza kwa chakula.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis wakati alipokutana na Balozi wa Cuba nchini, Yordaenis Despaigne aliyefika kwa ajili ya mazungumzo katika kuimarisha sekta ya kilimo.
Khamis alisema malengo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kujitosheleza kwa chakula na kupunguza uagizaji wa chakula nje ya nchi ikiwemo mpunga.
Alizitaja juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwemo ujenzi wa miundombinu katika mashamba ya mpunga ambayo ni pamoja na ujenzi wa visima vya kuzalisha maji na kusambaza katika mashamba ya wakulima.
”Mikakati yetu ni kujitosheleza kwa chakula na kupunguza uagizaji wa vyakula nje ya nchi ikiwemo mpunga ambapo tunatekeleza mradi wa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji mashambani,” alisema.
Aidha, kwa upande wa mazao ya viungo, alisema Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na taasisi za kimataifa ikiwemo Jumuiya ya Ulaya (EU) ambayo imeanza kuwashajihisha wakulima kilimo cha viungo.
Alisema Zanzibar katika miaka ya 1960 ilikuwa maarufu zaidi duniani kwa uzalishaji na usafirishaji wa mazao ya viungo ikiwemo pilipili manga, uzile pamoja na mdalasini.
Alisema kwa sasa wakulima wengi wamehamasika na kuanza kujikita katika kilimo cha vanila ambalo bei yake katika soko la ndani na nje ni nzuri yenye tija kwa wakulima.
”Tumeanza kuwashajihisha wakulima wetu hadi vijijini kuongeza uzalishaji wa mazao ya viungo ambayo soko lake lipo la uhakika kimataifa,” alisema.
Mapema Balozi wa Cuba nchini, Despaigne alisema nchi yake na Zanzibar ni marafiki ambayo imekuwa mstari wa mbele kusaidia Zanzibar katika sekta mbalimbali ikiwemo ya afya.
Kwa upande wa sekta ya kilimo, alisema Cuba imepiga hatua kubwa ikiwemo uzalishaji na usafirishaji wa mazao ya viungo na kuingiza kipato kikubwa kwa taifa na wakulima.
Alisema nchi yake ipo tayari kusaidia sekta ya kilimo ikiwemo cha umwagiliaji maji mashambani pamoja na mpunga hatua ambayo itaipunguzia mzigo serikali kuagiza vyakula nje ya nchi.
”Cuba tupo tayari kusaidia maendeleo ya Zanzibar zaidi katika sekta ya kilimo cha umwagiliaji maji pamoja na mazao ya viungo kwa ajili ya kuongeza usafirishaji nje ya nchi,” alisema.
Serikali ya Cuba imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia maendeleo ya sekta ya afya ambapo zaidi ya madaktari 10 wapo nchini huko wakisoma masomo ya fani mbalimbali wakati kwa upande wa Zanzibar wapo madaktari 12 kutoka Cuba wakitoa huduma za afya katika hospitali za Unguja na Pemba.