SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetoa shilingi bilioni 36 kuwezesha wavuvi wadogo, wakulima wa mwani, wafugaji wa kaa, wafugaji wa majongoo bahari na wakoshaji wa dagaa ikiwa ni sehemu ya mikakati ya uchumi wa buluu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Dk Aboud Jumbe amesema uwezeshaji huo ni sehemu ya fedha ilizopata SMZ kutoka kwenye mkopo uliotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kukabili athari za janga la Covid-19.
Dk Jumbe alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) katika Ofisi za Makao Makuu ya Kampuni hiyo Tazara, Dar es Salaam.
“Katika masuala ya uvuvi mdogomdogo wananchi wengi hawana uwezo wa kwenda nje ya kilomita mbili au tatu kwa sababu wana vidau, wana ngalawa sasa ukafanya vitu badala ya ngalawa na vidau ukaweka boti nzuri yenye mashine na kwenda kilomita sita au saba pamoja na mitambo ya kutafuta samaki na kumpa mvuvi aende akatafute samaki wapo wapi, utakuwa umewekeza,” alisema.
Dk Jumbe aliongeza: “Hivi sasa wavuvi wetu wanakwenda kuvua kwa kuangalia mwezi, upepo, maji lakini ukishakuwa na mifumo ya mawasiliano inajulikana samaki walipo. Lakini wewe ukishakuwa na ile mifumo ya mawasiliano itajulikana samaki wapo wapi.”
Alisema kila nchi katika uchumi wa buluu una malengo yake, lakini Zanzibar imeona iwawezeshe wananchi wake waweze kufanya shughuli zao kwa urahisi katika kuwasaidia kuwapa uelewa, mbinu, zana, mitaji na masoko katika maeneo yao ya uvuvi mdogomdogo.
Pia maeneo yao ya ufugaji wa kaa, ufugaji wa kamba, ufugaji wa pweza kwa kuwa hayo ni mambo ambayo yanajenga familia, yanajenga kaya, yanajenga jamii yanatengeneza mfumo mzuri wa mustakabali wa taifa katika kuwapa hao wajasiriamali uwezo.
“Tanzania dhana yake ni kumwezesha Mtanzania ambaye kila siku anahangaika na maisha sisi hatuwezi kuifikia dhana ya uchumi wa buluu ikaingia majumbani mwa watu ikiwa mwananchi mwenyewe hajaelewa faida ya dhana hiyo lakini pia haoni jitihada za serikali ya kumsaidia.”