WIZARA ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imependekeza kuingizwa kwa somo la maadili katika mitaala ya shule za Msingi na Sekondari.
Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ akizungumza bungeni leo Aprili 18,2023, amesema somo hilo litaingizwa kwenye mitaala ya shule na kufundishwa kwa lazima, ili kukabiliana na mmomonyoko wa maadili nchini.
Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Bahati Ndingo, aliyetaka kujua mkakati wa serikali kuhakikisha jamii inarudi katika maadili mema kutokana kutokana na ongezeko la mmomonyoko wa maadili nchini.
Naibu Waziri huyo amesema tayari wizara imechukua hatua mbali mbali za kukabiliana na hali hiyo, ikiwemo kuandaa mwongozo wa maadili na utamaduni wa mtanzania uliozinduliwa Julai 2, 2022 na unaendelea kusambazwa.
Amesema pia, serikali inaendelea kutoa elimu ya maadili na kufanya uhamasishaji wa mabadiliko ya fikra na vitendo kwa jamii kupitia vyombo vya Habari, mathalani katika kipindi cha Januari hadi April, 2023 Wizara imefanya vipindi 11.
“Pia Maafisa Utamaduni kutoka halmashauri 16 kati ya halmashauri 184 nchini wamefanya vipindi 21 kupitia vyombo vya habari vya kijamii,” amesema.
Amesema wanaendelea kutoa elimu ya maadili kwa wadau wa malezi na makuzi ikiwemo viongozi wa dini, wamiliki wa vituo vya malezi na shule za awali na wasanii
.
Amesema, Wizara inaandaa mdahalo na semina maalumu kwa wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wakati wa Tamasha la pili la Kitaifa la Utamaduni litakalofanyika mkoani Njombe Mei 19 hadi 21, 2023.