Spika: Benki ni tatizo Mikopo ya asilimia 10

DODOMA; SPIKA wa Bunge, Mussa Zungu, amesema benki nyingi nchini ndiyo tatizo kuhusu mikopo asilimia 10 ya halmashauri kuwafikia walengwa.

Spika Zungu ametoa kauli hiyo bungeni leo Februari 6, 2026, baada ya majibu ya serikali kwenye swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu Neema Majule aliyehoji serikali ina mpango gani wa kuanzisha mfumo madhubuti wa kupima matokeo ya mikopp hiyo ili kubaini changamoto na mafanikio.

Hata hivyo baada ya majibu ya serikali, Spika alisema serikali imefanya vizuri, watendaji serikalini pia wamefanya vizuri isipokuwa tatizo kubwa ni kwenye benki ambao wameweka masharti magumu yasiyotekelezeka kwa vikundi mbalimbali.

Amesema beki zikiendelea hivyo zitakwamisha juhudi za serikali na maana nzima ya mikopo hiyo itapotea.

Awali akijibu swali la msingi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Reuben Kwagilwa alisema kanuni za 31, 32 na 36 za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu za mwaka 2024 zinaelekeza na kuweka utaratibu wa kufanyika kwa tathmini ya utoaji na usimamizi wa mikopo kila mwaka katika ngazi ya halmashauri, mkoa na taifa.

“Ofisi ya Waziri Mkuu – Tamisemi imekwishafanya tathmini mara moja tangu kuanza kwa mfumo mpya wa utoaji mikopo.

“Pia tathmini imekuwa ikifanyika kulingana na changamoto ambazo zinajitokeza wakati wa utekelezaji. Tathmini hizi ndizo zinawezesha kufanya maboresho mbalimbali mifumo inayotumika,” amesema na kuongeza:

“Hadi kuishia Januari, 2026, jumla ya vikundi 24,064 vimepata mikopo, ambapo vikundi vya wanawake ni 13,639, vijana ni 8,140 na watu wenye ulemavu ni 2,285.

Serikali pia imejenga uwezo kwa wasimamizi 736 wa halmashauri na 78 wa mikoa kuhusu usimamizi wa Mfumo wa Wezesha, na inaendelea kuufanyia maboresho ili kuongeza ufanisi na tija ya mikopo kwa wananchi,” amesema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button