TANGU mwaka 1963, Serikali ya Sweden na Tanzania zimeendelea kudumisha diplomasia kwa taifa hilo lililopo Ulaya ya Kaskazini kuipa Tanzania misaada mbalimbali yenye thamani ya zaidi ya Dola bilioni nane hadi kufikia mwaka huu.
Balozi wa Sweden nchini, Charlotta Ozaki Macias alisema hayo alipozungumza waandishi wa habari mjini Morogoro baada ya kuwatembelea Wananchi waliopatiwa msaada wa kisheria na kituo cha wasaidizi wa kisheria Mkoa wa Morogoro jana.
Wengi waliopatiwa msaada wa kisheria ni wanawake ambao walikuwa na kesi mahakamani za kupigwa na wenza wao, kesi za ndoa na kudhulumiwa mali ambapo kituo hicho kinawatumia mawakili na wanasheria kupitia ufadhili wa ubalozi wa Sweden nchini.
Balozi Macias alisema nchi yake ni mchangiaji mkubwa wa misaada kwa Tanzania na katika maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzisha ubalozi wake mwaka 1963 hadi kufikia mwaka 2023 imetoa ufadhili wa kiasi hicho cha fedha kwa Tanzania.
Alisema ufadhili huo umetolewa katika sekta mbalimbali kuanzia za elimu ya msingi, ufundi, vyuo vikuu na elimu ya watu wazima kupitia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC).
Alisema mpango FDC ulianzishwa mwaka 1970 ambao unaendelea na umekuwa wa mfano mzuri kuchangia maendeleo ya elimu chini Tanzania.
Eneo lingine ni kwenye kusaidia mpango wa uendelezaji wa usambazaji umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuchangia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ikishirikiana na nchi za Jumuiya ya Ulaya (EU) pamoja na eneo la viwanda vidogo chini ya Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO).
Ofisa wa Ubalozi anayeshughulikia Asasi za Kiraia, Habari na Elimu, Stephen Chimalo alisema katika kuelekea miaka 60 ya Ubalozi Sweden nchini, umeendelea kuiwezesha Tanzania kwenye ufadhili katika nyanja za kielimu, kilimo, sekta ya umeme na huduma za kijamii.
Chimalo alisema katika kusherehekea miaka 60 ya tangu kuanzisha ushirikiano wa kibalozi na Tanzania, ulianza kutembelea Tawi la shirika lisilo la kiserikali la The Tanzania Human Rights Defenders Coalition (THRDC) lililopo Dar es Salaam ambao ni watetezi wa haki za binadamu.
Alisema shirika hilo katika utendaji wake wa kazi linafanya na makundi madogo ya wasimamizi wa kisheria likiwemo la Morogoro Paralegals ambao ni wanasheria wasiosomea ambao wanatambulika kwa udogo wao waweza kutafsiri sheria zilizopo nchini na kuwasaidia wanajamii waliopo vijijini .
“Balozi na ujumbe wake umetembelea Ofisi za Paralegal Centre na inafanya kazi kwa kuwatumia wanasheria wao wadogo kuwasaidia wananchi wenye kesi zao mbalimbali zinazowasibu, akina mama waliopitia maumivu makali ambao huku nyuma walifika katika ofisi hizo kutoa taarifa “ alisema Chimalo
“ Hii ni safari ya kusherekea miaka 60 ya maendeleo na biashara ambapo nchi hiyo inashirikiana na Tanzania na kilele cha maadhimisho haya ni kwa safari hiii pekee ambayo imeanzia kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, lakini maadhimisho hayo yanaendelea kwa mwaka mzima mpaka Disemba 31, 2023 ndiyo itakuwa ni kilele cha mwisho” alisema Chimalo
Chimalo alisema Ubalozi wa Sweden nchini Tanzania haufanyi kazi moja kwa moja na wananchi , bali ubalozi huo unafanya kazi kwa kupitia asazi za kiraia na taasisi za serikali ambazo kwa wastani zinafikia 60.
Wanufaika waliopatiwa msaada wa kisheria na kituo cha wasaidizi wa kisheria Mkoa wa Morogoro waliishukuru ubalozi huo kwa ufadhili wanaoutoa katika kuwawezesha wananchi wasio na uwezo kumudu uendeshaji wa kesi na kupata haki zao .