Taasisi elimu, dini zatakiwa kulinda maadili
TAASISI za elimu kuanzia ngazi ya chini, mpaka elimu ya juu kwa pamoja na taasisi za dini zimetakiwa kurithisha mila na desturi lengo kukabiliana na mmomonyoko wa maadili.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumaro ametoa agizo hilo alipozungumza na wananchi mbalimbali katika ufunguzi wa tamasha la tatu la utamaduni kitaifa uwanja wa Majimaji Songea mkoani Ruvuma leo.
Akizungumzia suala la maadili, Dk Ndumbaro amesema taasisi za dini zinapaswa kuwa na mchango mkubwa kupambana na suala hilo, hata hivyo amevitaka vyombo vya habari na watu maarufu kuwa sehemu ya kupambana na vita ya maadili.
SOMA: Samia asisitiza maadili bora kwa watoto
“Tuwafundishe maadili mema watoto wetu, viongozi wa dini mna jukumu kubwa sana, kwa sababu kupitia ninyi watu wengi wanaweza kujifunza maadili, na maadili mengi ya dini ndio yanatusaidia taifa letu kuwa na utamaduni wake,” amesema Dk Ndumbaro.
Ufunguzi wa Tamasha la tatu la Utamaduni la Kitaifa Mkoani Ruvuma Septemba 20, 2024.
Waziri Ndumbaro tayari amewasili Uwanja wa Majimaji Songea kwa ajili ya ufunguzi wa Tamasha hilo. pic.twitter.com/rFr0yYui51
— Wizara ya Sanaa (@WizaraSanaa) September 20, 2024
Dk Ndumbaro ameiomba Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kuwachukulia hatua watakaohusika au kubainika kuwa sehemu ya mmomonyoko wa maadili kupitia mitandao ya kijamii.
SOMA: fanyeni tafiti za masuala ya malezi na maadili
Akizungumzia tamasha hilo, Dk Ndumbaro amesema tamasha hilo lina umuhimu wa kipekee, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 ambayo inataka wizara yenye dhamana ya sanaa, utamaduni na michezo kuenzi, kukuza, kuendeleza na kudumisha utamaduni wa Mtanzania.
“Pili kama nilivyosema ni utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Rais ambayo aliyatoa kule Mwanza 2021,” amesema Dk Ndumbaro.
Tamasha la Utamaduni la Kitaifa mkoani Ruvuma ni tukio linalosherehekea na kuonesha utajiri wa utamaduni wa Kitanzania, likiwaleta pamoja washiriki kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania kushindana na kuonyesha vipaji vya ngoma, muziki, sanaa, na desturi za jadi.