Tabaka la Ozoni laanza kuimarika

NEW YORK , MAREKANI : RIPOTI mpya ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), chini ya Umoja wa Mataifa, imeonesha kuwa tabaka la ozoni linaendelea kurejea taratibu katika hali yake ya asili baada ya juhudi za kimataifa kudhibiti gesi chafu.
Tabaka la ozoni ni kinga muhimu inayolinda uso wa dunia dhidi ya miale hatarishi ya jua, ambapo kuyumba kwake kulitajwa kuanza miaka zaidi ya 40 iliyopita. Ripoti ya WMO imeeleza kuwa tundu lililojitokeza kwenye tabaka hilo limeanza kupungua ukubwa wake na kunatarajiwa kutoweka kabisa katika miongo ijayo. SOMA: Umuhimu soko la kaboni kukabili mabadiliko tabianchi
Miaka ya 1980, wanasayansi walionya kuhusu kuharibika kwa tabaka hilo na athari zake, ikiwemo ongezeko la joto duniani. Tangu hapo, mataifa yamechukua hatua za pamoja kupunguza matumizi ya vifaa vinavyotoa gesi chafu, vikiwemo majokofu na viyoyozi.



