NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi, amemtaka Kamanda wa TAKUKURU wilayani Ruangwa, kufanya uchunguzi wa matumizi ya kiasi cha Sh Milioni 102 zilizotolewa na Serikali kupitia TASAF, ili kujenga zahanati katika Kijiji cha Mtakuja wilayani Ruangwa na kuwasilisha taarifa ya uchunguzi huo kwake kabla ya kuhitimisha ziara yake mkoani Lindi.
Ndejembi ametoa maelekezo hayo kwa kamanda wa TAKUKURU Wilaya ya Ruangwa, mara baada ya kukagua na kutoridhishwa na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Mtakuja, akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Ndejembi amesema, amesikiliza kwa makini taarifa ya ujenzi wa zahanati hiyo iliyowasilishwa na mratibu wa TASAF Wilaya ya Ruangwa, lakini hajaridhishwa nayo kutokana na upungufu uliyomo, ikiwa ni pamoja na kiasi cha shilingi milioni 27 kilichoainishwa kubaki kwenye akaunti kati ya shilingi milioni 102 zilizotolewa na TASAF, hivyo hakitoweza kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo.
Naibu Waziri Ndejembi amemuelekeza Kamanda wa TAKUKURU kuhakikisha anafanya uchunguzi maalum na kumchukulia hatua yeyote akatayebainika kuhusika na ubadhirifu wa fedha za umma.
“Ni lazima tusimamie vizuri fedha za umma hususani za TASAF ambazo zinatafutwa na Mhe Rais Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya kuzikwamua kaya maskini kutoka katika lindi la umaskini, ni lazima kuwa na uchungu na matumizi mabaya ya fedha za umma,” amesema Naibu Waziri Ndejembi.