Takukuru yaonya rushwa, kuchafuana Uchaguzi Mkuu

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeonya wananchi kuwa wakichagua viongozi watoa rushwa hawatawajibika kwenye maendeleo yao kwa miaka mitano ijayo.
Pia, taasisi hiyo imetaka wagombea katika uchaguzi mkuu ujao wafanye siasa za kistaarabu, waache kuchafuana na kukomoana.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila amesema hayo wakati akifungua warsha kwa wadau wa habari Dar es Salaam kujadili namna ya kuzuia na kupambana na rushwa katika uchaguzi mwaka huu.
“Tunahimiza wananchi waepuke vitendo vya rushwa na wasikubali kuchangua viongozi wanaotoa rushwa kwa sababu hawana msaada wowote kwao kwa kipindi chote cha miaka mitano ijayo, hizi ni salamu na ujumbe tunaomba uwafikie wananchi,” alisema Chalamila.
Alisema wameanza kutoa warsha kwa wadau ili nao waende kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kufanya uchaguzi kwa umakini kwa lengo la kupata viongozi bora wanaowajibika.
“Rushwa ni saratani kubwa ambayo haiwezi kukabiliwa na sheria au taasisi moja, ni suala la ushirikishwaji wa wadau wote,” alisema Chalamila.
Alihimiza wananchi waepuke vitendo vya rushwa wakati wa maandalizi na siku ya uchaguzi wachague viongozi waadilifu kwa ajili ya maendeleo yao na taifa.
“Tunaamini kupitia waandishi wa habari, wanaweza kufanya habari za uchunguzi, kufichua vitendo vya rushwa na kusaidia vita ya mapambano na kusaidia jamii isipate viongozi wanaotokana na rushwa,” alisema Chalamila.
Alisema kuna umuhimu wa Takukuru kukutana na wadau kuwaelimisha kupinga vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi kwa wagombea.
Alihimiza wananchi pia wasiombe rushwa kwa wagombea. Chalamila alisema mwaka jana kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa kulikuwa na malalamiko ya wagombea na wapambe kuhusu vitendo vya rushwa.
“Kama taasisi, hatukurupuki kwenda kumkamata mtuhumiwa kwa vile tu malalamiko yametolewa, tunafungua jalada la uchunguzi na kuchunguza na katika kufanikisha kuchunguzi tunategemea sana msaada wa watoa taarifa ya walioibua waje washirikiane na sisi,” alisema Chalamila.
Alisema Takukuru iliwafuata kuwataka waeleze kuhusu tuhuma hizo za rushwa lakini hawakujitokeza na wengine pamoja na kupewa wito wa kwenda kutoa ushahidi dhidi ya watuhumiwa pia hawakujitokeza.
“Kwa masikitiko makubwa wengi hawakujitokeza na wengine hawakuitikia wito wetu kuja kutoa malalamiko yao na mwisho wa siku tukagundua ilikuwa kampeni chafu za uchaguzi miongoni mwa wagombea kuchafuana, mwisho wa siku tunawachanganya wananchi ambao wanaweza kumkosa kiongozi mzuri kama watashikilia vitu kama hivyo,” alisema Chalamila.
Aliwataka wanasiasa kuacha kuchafuana na kukomoana bali wafanye siasa za kistaarabu ili kupata viongozi bora.
Akizungumzia zawadi wakati wa uchaguzi, Chalamila alisema zinapaswa kuangaliwa kwa umakini.
“Kuhusu zawadi je unatoa muda gani, tunaishi wote eneo hili na hujawai kutoa zawadi iweje leo uje utoe zawadi ili hali umetangaza kugombea eneo hili hili, hizo zawadi lazima ziangaliwe,” alisema Chalamila.
Hata hivyo alisema ni vyema pia kutambua vitu gani si zawadi wakati wa kampeni. Akizungumzia mafunzo hayo, mhariri Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Tausi Mbowe alisema mafunzo hayo ni muhimu kwao kwa sababu wanajadili masuala mbalimbali kuhusu rushwa na jinsi ya kukabiliana nayo kuelekea uchaguzi mkuu.
“Wahariri ni wadau wakubwa katika uchaguzi na tuna wajibu wa kusaidia wananchi kuelewa na kuchagua viongozi kutokana na sera zao na si rushwa,” alisema Tausi.