Takukuru yawagusa wenye uhitaji Manyara

MANYARA: Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Manyara imekabidhi vyakula na zawadi mbalimbali kwa watoto yatima wanaoishi katika kituo cha kulelea watoto cha Hosana kilichopo wilaya ya Babati mkoani Manyara.
Kamanda wa TAKUKURU Manyara, Bahati Haule amesema vyakula na misaada ni michango ya watumishi na kwamba Iftar ni kiungo kati ya taasisi hiyo na wadau kukaa, kula na kupata nasaha kutoka kwa viongozi wa dini ili kujenga maadili na ustawi kwa jamii.
Aidha, amebainisha kwamba shughuli hiyo imetokana na utashi wa serikali na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila kuhimiza watumishi kuwa karibu na wananchi na kuwa raia wema ikiwa ni sehemu ya jamii.
Mkurugenzi wa Kituo cha kulea watoto yatima cha Hossana Home Care Foundation, Neema Munis alibainisha kwamba kituo kina watoto 30 wenye mahitaji yote ya kibinadamu hivyo jamii inapaswa kuigwa mfano kutoka TAKUKURU .
Dovin Dastani, Shadrack Amos watoto kutoka kituo cha Hossana wameishukuru TAKUKURU kwa kuwakumbuka kwa mahitaji muhimu ikiwemo kitoweo cha mbuzi Kuelekea siku za Idd na Pasaka.
Baadhi ya watumishi kutoka TAKUKURU Wilaya ya Kiteto na Simanjiro Shela Mwegilo na Bizati Hassano waliiomba jamii kutoa sadaka ya kugusa mioyo kwa wenye uhitaji. Vyakula vilivyotolewa ni mchele, mbuzi, viungo, sukari, mafuta ya kupikia, sabuni na maharage.



