TAMISEMI yaomba Sh trilioni 11.78 Bajeti 2025/26

DODOMA — Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imetangaza makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/26, ikitoa jumla ya Sh trilioni 11.783 kwa ajili ya wizara na taasisi zilizo chini yake.
Bajeti hii imeonekana kuongezeka kwa zaidi ya Sh trilioni 1.66, ikilinganishwa na ile ya mwaka 2024/25 ambayo ilikuwa Sh trilioni 10.125.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, alieleza kuwa kiasi cha Sh trilioni 3.95 kimeombwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ambapo Sh trilioni 2.5 zitakuwa ni fedha za ndani, ikiwa ni pamoja na Sh bilioni 613.44 za mapato ya ndani ya halmashauri. Sh trilioni 1.45 ni fedha za nje, zikiwa na lengo la kuendeleza miradi ya kimaendeleo katika maeneo mbalimbali.
Aidha, matumizi ya kawaida katika bajeti hiyo yamepangwa kuwa Sh trilioni 7.84, ikijumuisha mishahara ya watumishi wa umma yenye jumla ya Sh trilioni 6.3 na matumizi mengineyo ya Sh trilioni 1.53. Mchengerwa alisisitiza kuwa, kati ya fedha hizo, Sh trilioni 1.067 zitakuwa ni mapato ya ndani ya halmashauri.
“Hatutaki sifa za kisiasa, bali tunataka suluhisho sahihi kwa maisha ya Mtanzania wa kawaida,” Mchengerwa alisema, akisisitiza kuwa bajeti hii ni dira ya matumaini na ramani ya maendeleo kwa taifa. Aliendelea kusema kuwa TAMISEMI ni msingi wa maendeleo endelevu, ambapo kila shilingi ina jukumu na kila kiongozi ana wajibu.
Mchengerwa ametoa wito kwa mikoa, mamlaka za serikali za mitaa, na wananchi kushirikiana kwa pamoja ili kufanikisha malengo ya maendeleo.
Alisema, “Kwa imani kubwa katika maono ya Rais Samia Suluhu Hassan, bajeti hii ni zana ya kazi na silaha ya mapinduzi ya kiutawala, kiuchumi na kijamii.”