Tamisemi yatoa maagizo majanga ya moto

OFISI ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imewataka Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanafanya tathmini ya namna bora ya kukabiliana na majanga ya moto katika maeneo yao ili wawe na utayari wa kuyakabili pindi yanapojitokeza.

Maelekezo hayo yametolewa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI Deogratius Ndejembi kwa niaba ya Waziri wa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa kwenye ziara ya kukagua eneo la wafanyabiashara la Kariakoo ambalo liliungua na moto siku ya Oktoba mosi, 2023.

Ndejembi amewataka viongozi hao kuwa na utamaduni wa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Mazingira katika kuchukua hatua za dharura endapo likitokea janga la moto.

Pia ameagiza uongozi wa mkoa wa Dar es Salaam na wilaya unapaswa kushirikiana DAWASA kufanya tathmini ya kuepukana na majanga ya moto.

Aidha, Ndejembi amewaomba wafanyabiashara walioathirika na janga la moto kuwa wavumilivu hadi kamati ya uchunguzi iliyoundwa itakapotoa taarifa za chanzo cha janga la moto lililojitokeza.

“Wafanyabiashara kuweni wavumilivu mpaka kamati ya siku saba iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa itakapotoa taarifa rasmi ya janga hilo ili kuiwezesha Serikali sikivu ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuchukua hatua stahiki na kuongeza kuwa, zimebaki siku nne tu kamati hiyo ikamilishe taarifa,” amesisitiza Ndejembi

Aidha, Ndejembi amewasilisha salamu za pole za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mchengerwa kwa wahanga wa janga hilo la moto ambao wamepoteza mali zao na kupata hasara kibiashara.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
5 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
5
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x