Tamwa yatoa kongole kwa Rais Samia haki za watoto

Rais Samia Suluhu Hassan

CHAMA cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimewapongeza Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima kwa kuonesha msimamo imara kusimamia haki za watoto.

Aidha, kimesema wazazi, walezi, wanasheria, serikali na jamii kwa ujumla wanapaswa kuungana kuhakikisha watoto wanakingwa dhidi ya ukatili wanaofanyiwa ukiwamo wa kupitia mitandaoni.

Katika mazungumzo na HabariLEO Jumapili, Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Dk Rose Reuben kuhusu maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka huu, alisema: “Tamwa tunampongeza Rais Samia pamoja na waziri mwenye dhamana, ambao wanaonesha wazi kuwa wanasimamia vyema haki za watoto… tumewaona na kuwasikia wakipinga ukatili kwa watoto hivyo, hatuna budi kusimama nao katika hili.”

Advertisement

Aliutaja ukatili mwingine mbali na udhalilishaji kupitia mitandao kuwa ni pamoja na ndoa na mimba za utotoni, ulawiti, ubakaji, ukeketaji, unyanyapaa na ajira mbaya kwa watoto.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Mambo ya Ndani, tangu Julai 2022 hadi Mei 2023, mashauri 14,184 ya matukio ya ukatili kwa watoto yameripotiwa katika vituo vya Polisi ikilinganishwa na matukio 12,642 yaliyoripotiwa mwaka 2021/2022.

Siku ya Mtoto wa Afrika huadhimishwa kila Juni 16 na kutumika kuwakumbusha watoto hatua ya kijasiri waliyofanya wenzao wa Afrika Kusini mwaka 1976 kulinda haki zao na kuleta mabadiliko chanya hata wakiwa wadogo.

Awali kupitia taarifa iliyosainiwa na Dk Rose, Tamwa ilisema, “katika maadhimisho ya mwaka huu yenye kaulimbiu: ‘Zingatia Usalama wa Mtoto Katika Ulimwengu wa Kidijiti’, Tamwa tunahimiza jamii kuongeza ulinzi kwa watoto kwa kuwakinga dhidi ya ukatili ukiwemo wa mitandaoni, mimba za utotoni, ulawiti, ukeketaji, unyanyapaa na ajira mbaya kwa watoto.”

Kwa mujibu wa Dk Rose, kaulimbiu hiyo inasisitiza kuwalinda watoto na kuwaongoza katika matumizi sahihi ya kidijiti yakiwemo ya simu za mkononi, kompyuta na runinga kwa kuwa vitu hivyo vikitumika vibaya vinaweza kusababisha ukatili wa mitandaoni kwa watoto.

“Kila mtu katika jamii awe chachu kwa kutengeneza mazingira rafiki kwa watoto kutoa taarifa wanapoona viashiria vya ukatili vinavyofanywa na mtu yeyote katika mazingira atakayokuwepo mtoto yakiwemo ya mitandaoni,” alisema.