Tanzania, Burundi zampa mtu binafsi kujenga SGR

SERIKALI za Tanzania na Burundi zimeshasaini makubaliano ya kujenga Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Uvinza hadi Gitega kupitia machimbo ya nickel nchini Burundi ambapo mtu binafsi atajenga reli hiyo kutokana na nchi hizo kutokuwa na fedha kwa sasa.

Hayo yalibainishwa na Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu, Dar es Salaam jana wakati wa hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) Awamu ya Pili kipande cha sita kutoka Tabora hadi Kigoma chenye urefu wa kilometa 506.

Rais Samia alisema reli hiyo lazima ijengwe kwa kuwa Msongati kuna mzigo mkubwa wa madini hayo ambayo usafirishaji wake utategemea reli hiyo.

“Nataka niwape habari za faraja kwamba tayari kuna mtu ameshajitokeza anataka kujenga kwa fedha yake ambayo siyo mkopo halafu tutakatana kwenye usafirishaji wa mali yake atakapokuwa anasafirisha,” alisema.

Alisema wakati wowote mkataba wa ujenzi wa reli hiyo ya Uvinza kwenda Msongati kwenye nickel utasainiwa na mtu huyo anayejitolea kwa kuwa lengo ni kuunganisha Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, alisema utiaji saini wa ujenzi wa kipande cha reli kutoka Tabora hadi Kigoma unahitimisha ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha SGR kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma yenye jumla ya kilometa 2,102 na ujenzi utakaofuata ni matawi ya reli hiyo.

Kadogosa alisema kilometa hizo 2,102 unazifanya Tanzania kuwa nchi yenye ujenzi wa reli ndefu ya SGR Afrika na kuongeza kuwa mikataba yote iliyosainiwa ya ujenzi wa SGR haina mabadiliko ya bei kutokana na mabadiliko ya bei za bidhaa za ujenzi.

“Wakati tunaanza ujenzi tulikuwa na makadirio ya kujenga kilometa moja kwa dola za Marekani milioni 4.46 lakini mpaka sasa tumejenga kwa dola za Marekani milioni 4.06, kwa hiyo ujenzi wetu wote mpaka sasa upo chini ya makadirio ya kiuhandisi ya dola bilioni moja,” alisema.

Alisema kati ya nchi 22 zinazotekeleza miradi ya SGR, nchi 17 zinatoka Afrika na nchi ambayo imejenga kilometa 500 ambayo siyo ya SGR ya umeme inajenga kwa dola milioni 6.218 kwa kilometa, hivyo gharama ya ujenzi wa SGR kwa Tanzania ni nafuu.

Kuhusu ununuzi wa vitendea kazi, Kadogosa alisema ununuzi huo yakiwemo mabehewa 59 unaendelea vizuri na 14 kati ya hayo yameshawasili nchini, mabehewa mengine 30 na vichwa viwili ambayo yametumika yataingia Machi au Aprili mwakani.

Pia alisema kuna vichwa 17 kutoka Korea Kusini vitaanza kuingia Juni mwakani, seti 10 za treni za kisasa na seti mbili kati ya hizo zitaingia Juni, mabehewa ya mizigo 1,430 kutoka China yataanza kuingia Septemba mwakani na kufanya uwekezaji wote huo kuwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 557.731 sawa na Sh trilioni 1.29.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, alisema sekta ya ujenzi na uchukuzi ni mhimili wa maisha ya Watanzania.

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, aliiomba serikali baada ya kukamilisha ujenzi wa SGR, kuona namna ya kuboresha maeneo mengine yenye reli ya zamani nayo kuwa katika SGR.

Katibu Mkuu Uchukuzi, Gabriel Migire alisema kati ya mzigo wote unaopita Bandari ya Dar es Salaam, asilimia 39 ni mzigo wa DRC na ujenzi wa SGR utakapokamilika, mzigo huo utaongezeka kwa zaidi ya asilimia 50 lakini pia utasaidia uzalishaji wa tani milioni 150 za nickel nchini Burundi.

Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Jilly Maleko, alisema SGR kwenda Msongati nchini Burundi itasaidia usafirishaji wa tani 600,000 za nickel safi kwa mwaka kusafirishwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam na kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Burundi katika kipindi cha mwaka 2019/2020 kilikuwa kati ya dola bilioni 50 hadi 80.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Kichina ya CCECC, Zhang Junle, itakayojenga reli hiyo ya Tabora hadi Kigoma kwa ushirikiano na Kampuni ya CRCC alisema watakamilisha mradi huo kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa.

Aidha, Kadogosa alisema kuwa ujenzi wa SGR kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro umefikia asilimia 97.67 na mikoa mingine na asilimia zake kwenye mabano ni Morogoro-Makutupora (91.32), Makutupora-Tabora (3.26), Tabora-Isaka (0.49) na Isaka-Mwanza asilimia 19.70.

Habari Zifananazo

Back to top button