Tanzania, Cuba kupambana na maralia

PWANI: SERIKALI ya Cuba imeahidi kutoa ushirikiano kwa serikali ya Tanzania katika katika mapambano dhidi ya malaria.
Rais wa Bunge la Cuba, Esteban Hernandez ametoa ahadi hiyo leo Machi 5, 2025 alipotembelea kiwanda cha Tanzania Biotech Products Limited kinachozalisha viuatilifu kilichopo wilayani ya Kibaha, mkoani Pwani.
Kiwanda hicho kilichojengwa kwa gharama ya takriban Dola milioni 22.3, kinajihusisha na uzalishaji wa viuatilifu vya kupambana na vimelea vya wadudu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vimelea vinavyosababisha malaria.
Soma zaidi: Watafiti Cuba wafanya ziara Serengeti
Hernandez amesema kuwa ushirikiano huo umetokana na mafanikio ya kiwanda hicho nchini Cuba, ambapo ameeleza kuwa kutumia bidhaa za kiwanda hicho kutasaidia kudhibiti ugonjwa wa malaria na kulinda afya ya wananchi wa Tanzania.

“Msingi mkubwa wa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanakuwa salama dhidi ya magonjwa mbalimbali, ikiwemo malaria. Huu ni mfano mzuri wa utayari wa serikali ya Cuba katika kusaidia kupambana na madhara yanayosababishwa na malaria. Natoa hakikisho kwamba serikali ya Cuba ipo tayari kuisaidia Tanzania katika vita hii dhidi ya malaria,” amesisitiza Hernandez.
Soma zaidi: Serikali kuajiri walimu wa ngumi wa Cuba
Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Hamphrey Polepole amesema serikali ya Tanzania imeweka jitihada katika kupambana na malaria na kuokoa maisha ya wananchi. Amezitaka halmashauri zote zinazopokea viuatilifu kutoka kiwanda hicho kutumia bidhaa hizo kwa mujibu wa maelekezo ya kitaalam ili kupata matokeo bora.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Suleiman Serera ameeleza kuwa kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha lita milioni 1.2 za viuatilifu, ingawa uwezo halisi wa kiwanda ni kuzalisha hadi lita laki sita.
Amesisitiza kuwa serikali imetenga kiasi cha Sh bilioni 10 kwa ajili ya kununua bidhaa zitakazozalishwa na kiwanda hicho kwa matumizi ya ndani kabla ya kuzipeleka nje ya nchi.
“Kiwanda hiki ni muhimu sana kwa taifa letu, na uwezo wake wa uzalishaji ni mkubwa. Mwaka huu, serikali imetenga takriban shilingi bilioni 10 kuhakikisha kwamba bidhaa zinazotoka hapa zinanunuliwa na kutumika nchini,” amesema Dk. Serera.
Nicholas Shombe, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), amebainisha kuwa kiwanda hicho ni cha pekee barani Afrika na kimefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kupambana na malaria. Aidha, kiwanda hicho kinauza bidhaa zake kwa nchi nane za Afrika.
Pia, Shombe ameongeza kuwa kiwanda hicho kinatarajia kuzalisha mbolea salama kwa matumizi ya wakulima, ambayo itakuwa haina sumu na itawezesha wakulima kuuza mazao yao kwa urahisi, hata katika masoko ya kimataifa.



