Tanzania, Denmark kushirikiana kilimo, Uchumi wa Buluu

Katika jitihada za kukuza na kuendeleza diplomasia ya uchumi, Serikali za Tanzania na Denmark zimeahidi kuendelea kushirikiana katika sekta za uchumi wa Buluu pamoja na kilimo.
Makubaliano hayo yamefikiwa wakati Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, alipokutana na Balozi wa Denmark nchini, Mette Norgaard Spandet katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Waziri Mulamula ameeleza kuwa ushirikiano wa Tanzania na Denmark ni wa muda mrefu na wa kihistoria, hivyo Tanzania itaendeleza ushirikiano huo kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa maslahi ya mataifa yote mawili.
Pamoja na mambo mengine, Waziri Mulamula amemuelezea Balozi Spandet juu ya fursa mbalimbali, ambazo ziko Tanzania katika kukuza sekta za uchumi wa buluu na kilimo.
“Tanzania inazo fursa nyingi katika sekta ya Uchumi wa Buluu ikiwemo uvuvi, idadi kubwa ya samaki na wa aina mbalimbali, ambapo ni fursa ya kibiashara, tunazikaribisha kampuni za Denmark kuwekeza kupitia sekta hiyo,” amesema Balozi Mulamula.
Viongozi hao pia wamejadili njia za kuboresha sekta ya kilimo nchini, ili kuwawezesha Watanzania wengi kunufaika na sekta hiyo, hasa ikizingatiwa kuwa asilimia kubwa ya Watanzania hutegemea kilimo.
Kwa upande wake Balozi, Spandent ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wake na Denmark na kuahidi kuendelea kuudumisha ushirikiano huo katika sekta za kilimo, biashara na uwekezaji, tehama, utalii, demokrasia na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi.