MAMLAKA nchini zimeanza kufanya kazi na mashirika ya kimataifa ikiwa ni pamoja na Kituo cha Sayansi na Mazingira cha India (CSE) ili kukabiliana na taka ngumu ambazo zinazidi kuhatarisha afya na mazingira kwa ujumla.
Akizungumza leo Agosti Mosi, katika kikao cha wadau wa mazingira jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Immaculate Semesi amesema baraza kwa kushirikiana na CSE limedhamiria kusaidia urejelezaji wa taka ngumu kwa maeneo ya Dar es Salaam kabla ya kuhamia mikoa mingine.
SOMA: Kituo cha kurejeleza taka kujengwa Dodoma
“Tunataka taka ngumu igeuke kuwa fursa. Tunaitaka Dar es Salaam ifanikishe mpango huu kabla haujaanza katika mikoa mingine,” Dk Immaculate Semesi alisema na kuongeza kuwa: “Udhibiti wa taka ngumu bado ni changamoto na kama halmashauri tunaangalia afua mbalimbali ili kukabiliana na tatizo hilo.
Takwimu zinaonyesha Tanzania inazalisha zaidi ya tani milioni 17 za taka ngumu kila mwaka, ambapo chini ya asilimia 50 hukusanywa na kupelekwa dampo. Jijini Dar es Salaam, taka ngumu huchangia asilinia 55 ya gesi ya ‘methane’ inayozalishwa mkoani hapa.
Kati ya mwaka 2024 mpaka 2040, uzalishaji wa ‘methane’ unakadiriwa kuongezeka kwa zaidi ya asilimia 90. Hata hivyo wataalamu wanasema, Methane ni gesi chafu yenye nguvu ambayo ina hatari mara 80 zaidi ya ‘Carbon dioxide’ katika kipindi cha miaka 20.
Dk Semesi anasema baraza limejipanga kuzisaidia halmashauri ili kutekeleza kanuni bora. Kikao hicho kilikuwa na wawakilishi kutoka TAMISEMI, na halmashauri tano zinazounda Mkoa wa Dar es Salaam.
Katibu wa Pili wa Kamisheni Kuu ya India nchini, Nerender Kumar alisifu ushirikiano kati ya NEMC na CSE ya India akisema shirika hilo limekuwa likifanya kazi na taasisi za Kusini ili kuimarisha uwezo na kusaidia kukabiliana na changamoto za sasa za mazingira.
Mkurugenzi wa Programu (Bodi & Ufadhili) wa CSE, Aditya Batra alisema kituo hicho kinafanya kazi na mataifa mbalimbali Afrika na Asia katika kusaidia kutafuta afua nafuu ya kukabiliana na changamoto ya mazingira.