Tanzania iweke maeneo ya kihistoria ya Papa Leo XIV

DODOMA; Spika wa Bunge. Mussa Zungu amesema kuna haja serikali ikaweka maeneo ya kihistoria Tanzania, ambayo Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Leo XIV aliishi alipokuwa nchini Tanzania.
Spika Zungu ametoa kauli hiyo leo Februari 6, 2026, muda mfupi baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Prof Kitila Mkumbo kumaliza kufanya majumuisho ya hoja mbalimbali za wabunge kwenye hotuba yake kuhusu Mpango Elekezi wa Muda mrefu wa miaka 25 (2026/27 hadi 2050/51), Mpango wa Nne wa Maendeleo wa miaka mitano (2026/27 hadi 2030/31) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2026/27.
Amesema Papa Leo ameishi Tanzania na amekuja mara kadhaa maeneo ya Morogoro, Dar es Salaam na Songea mkoani Ruvuma, lakini wengi hawajui kuhusu historia hiyo.
Amesema wapo marafiki wa Papa Leo, zipo nyumba alizoishi na hata mabenchi aliyokuwa anakalia kanisani, ni vyema vikawa sehemu ya kutengeneza maeneo ya historia ili kuvutia watalii wa kidini wanaokuja nchini.
HabariLEO ilipata kutoa makala maalumu kuhusu Papa Leo XIV, ikieleza kwa miaka tofauti aliwahi kufika Tanzania na kupita maeneo kadhaa ikiwemo Dar es Salaam, Morogoro, Njombe na katika nyumba ya malezi ya shirika hilo iliyopo Mahanje Jimbo Kuu Katoliki la Songea.
Isome pia:https://habarileo.co.tz/papa-leo-xiv-mwenyeji-tanzania/
Katika makala hayo Askofu wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo, Stephano Musomba ambaye ni mwanashirika wa Mtakatifu Augustino (O.S.A), alikaririwa akisema kwa mara ya kwanza alimuona Papa Leo XIV nchini mwaka 2003 alipokuwa mkuu wa shirika hilo.
“Papa Leo XIV alikuja Tanzania mwaka 2003, kutembelea jumuiya za Waagustino Tanzania yeye akiwa mkuu wa shirika ulimwenguni. Na kati ya shughuli alizozifanya, alikuja akafikia kwenye nyumba yetu ya Mahanje kule Songea,” alisema Askofu Musomba.
–
Alisema kama mkuu wa shirika alikuwa na wajibu wa kutembelea jumuiya zote za shirika hilo na kwa Tanzania walikuwa na nyumba ya malezi huko Mahanje, Songea mkoani Ruvuma, Morogoro na Parokia ya Mavurunza, Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
–
“Tulipanda gari moja na Papa Leo (akiwa mkuu wa shirika) na mimi ndiye niliendesha gari kutoka Songea mpaka Morogoro,” alikaririwa Askofu Musomba.



