Tanzania kupaa kimataifa uandaaji takwimu

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango ,Hamad Hassan Chande

OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS), inakusudia kuifikisha Tanzania kimataifa kwa kuongoza uandaaji wa takwimu bora.

Hatua hiyo inatokana na serikali kuidhinisha mpango wa pili wa kuimarisha na kuboresha takwimu ikiwa ni pamoja na kujenga na kuimarisha miundombinu ya kitakwimu.

Mtakwimu Mkuu wa Serikali , Dk Albina Chuwa amesema hayo Mei 21,2023 wakati wa kikao cha tatu cha baraza la sita la wafanyakazi wa ofisi ya takwimu kilichofanyika mkoani Morogoro.

Advertisement

Dk Chuwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa baraza la wafanyakazi wa Ofisi hiyo amesema kuwa, malengo ya mpango wa kwanza yaliifanya Tanzania kuwa nchi ya pili bora kati ya nchi 54 za Bara la Afrika katika uzalishaji wa takwimu.

Amesema kutekelezwa kwa mpango huu wa pili unakwenda kubadili kabisa tasnia ya takwimu nchini, na kuweza kulinganishwa na nchi nyingine yoyote bora ulimwenguni.

Kwa upande Naibu Waziri wa Fedha na Mipango ,Hamad Hassan Chande amesema serikali imeridhia utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Kuboresha na Kuimarisha Takwimu Tanzania.

Mpango huo unalenga kuboresha upatikanaji wa taarifa za kitakwimu za kiutawala ili kuwa na mifumo ya uhakika na ya gharama nafuu ya kuzalisha Takwimu nchini.

Chande amesema kuwa mpango huo ni miongoni mwa jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita za kujenga mazingira mazuri ya uzalishaji Takwimu nchini ambayo yataifanya NBS kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

“serikali itahakikisha inaongeza matumizi ya teknolojia katika ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu ili NBS itekeleze majukumu yake ipasavyo”amesema Chande

Chande amesema hatua ambayo inachagizwa na matokeo ya Tanzania kuteuliwa kuingia kwenye kamisheni ya takwimu ya umoja wa mataifa kwa kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2024 hadi 2027.

Naibu Waziri amesema kuwa, baada ya uzinduzi wa matokeo ya mwanzo ya sensa, umezifanya nchi za jirani ikiwemo Uganda kuja kujifunza mbinu na kanuni zilizotumika katika sensa ya watu na makazi mwaka 2022 ambayo ni ya kwanza kufanyika nchini kwa kutumia teknolojia ya kidijitali ya kisasa zaidi.

Awali , Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi upande wa Zanzibar, Balozi Mohamed Ally Hamza,amesifu ushirikiano wa wafanyakazi wa NBS nchini na kuweza kufanikisha zoezi la sensa ya Watu na Makazi Kwa kiwango cha ubora wa hali ya juu.