Tanzania, Marekani kushirikiana kukabili ugaidi

SERIKALI ya Marekani imesema itaendelea kushirikiana na Tanzania katika vita dhidi ya ugaidi.

Makamu wa Rais wa nchi hiyo, Kamala Harris amesema Marekani itafanya hivyo ili kuhakikisha ardhi ya Tanzania na ya Marekani inakuwa sehemu salama kwa wananchi wa nchi zote mbili.

Kamala alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waliokuwa wafanyakazi wanane wa ubalozi wa Marekani walionusurika katika shambulizi la kigaidi lililotokea Agosti 7, 1998.

Baada ya kuzungumza nao, Kamala aliweka shada la maua katika mnara wenye majina ya Watanzania 11 waliopoteza maisha katika tukio hilo.

Alisema bado Marekani inawathamini wafanyakazi hao ikiwa ni miaka karibu 25 tangu tukio hilo kutokea na kuongeza kuwa huzuni ya tukio hilo si ya Watanzania peke yao bali ni pamoja na Wamarekani wote.

“Marekani imesimama na Tanzania katika kuomboleza vifo vya Watanzania 11 ambao walikuwa watumishi wa Ubalozi wa Marekani, na itaendelea kutoa ushirikiano kwa Tanzania katika kutokomeza ugaidi duniani,” alisema Kamala.

Balozi wa Marekani wakati shambulizi hilo likifanyika mwaka 1998, Charles Stith alisema lilikuwa tukio la kutisha na anaishukuru Serikali ya Tanzania wakati huo ikiongozwa na Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa kwa ushirikiano alioutoa kukabili tukio hilo.

Balozi Stith alisema sababu ya kujenga mnara wa kumbukumbu ya tukio hilo ni kuwaenzi Watanzania 11 waliokufa na waliojeruhiwa na kuendeleza urafiki uliopo kati ya Tanzania na Marekani.

“Ujio wa Makamu wa Rais katika Bara la Afrika hususani Tanzania ni ishara kuwa Rais Joe Biden atatoa kipaumbele kwa Afrika pamoja na kuthamini ushirikiano na urafiki mzuri uliopo kati ya Marekani na Tanzania,” alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Noel Lwoga alisema ujio wa Makamu wa Rais wa Marekani umechangiwa kwa kiasi kikubwa na juhudi kubwa anayoifanya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha diplomasia na ushirikiano na mataifa duniani.

Lwoga alisema Makumbusho ya Taifa imekuwa kiunganishi cha urafiki kati ya Tanzania na mataifa mengine duniani hali ambayo imechangia kuimarisha utalii wa nchi.

Alisema ili kuwaenzi waathirika wa tukio hilo, Tanzania ilianzisha ushirikiano na Marekani katika vita dhidi ya ugaidi.

Mkurugenzi wa Kituo cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni, Adelite Salema alisema Makumbusho ya taifa ni kituo mama kati ya vituo saba vya makumbusho vilivyoko nchini.

Alisema makumbusho ya taifa inaeleza wazi kuwa uhusiano wa Tanzania na Marekani ulianza tangu mwaka 1961 wakati Baba wa Taifa alipofanya ziara ya kumtembelea Rais wa Marekani wakati huo, John F Kennedy mwaka 1961.

Kamala aliwasili juzi saa 5:05 usiku katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) akiwa amefuatana na mumewe, Douglas Emhoff.

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alimpokea kiongozi huyo akiwa amefuatana na mkewe, Mbonimpaye Mpango na viongozi wengine wa serikali.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button