TANZANIA ipo mbioni kuanza uzalishaji wa madini ya Niobium ambayo ni moja ya madini adimu yanayotumika katika mitambo mbalimbali ikiwemo matumizi ya utengenezaji wa injini za Ndege na Roketi.
Naibu Waziri wa Madini Dk Steven Kiruswa amesema hayo leo Oktoba 31 bungeni Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbeya Vijijini Oran Njema aliyetaka kujukua lini uzalishaji wa madini ya Niobium na kiwanda cha uzalishaji wa Ferroniobium utaanza katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.
SOMA: Wizara ya Madini waja kisasa zaidi
Dk Kiruswa amesema, mradi wa uchimbaji wa madini ya Niobium katika eneo la Panda Hill unamilikiwa na kampuni ya Panda Hill Tanzania Limited (PHTL) kwa ajili ya uzalishaji wa mazao yanayotokana na madini hayo ikiwemo zao la madini ya ferroniobium linalotokana na uchakataji wa madini ya Niobium.
Aidha, Dk Kiruswa ameongeza kuwa, tayari Serikali imeanza majadiliano na kampuni ya Panda Hill kwa lengo la kusaini Mkataba wa Makubaliano utakaowezesha Serikali kupata umiliki wa hisa kwenye mradi huo ikiwa pamoja na manufaa mengine ya kiuchumi.
Akielezea kuhusu hisa za Serikali katika mradi huo, Dk Kiruswa amesema kwa mujibu wa Sheria ya Madini, Sura ya 123, wamiliki wa Leseni za Kati na Kubwa za Uchimbaji Madini wamepewa sharti la kutoa hisa huru zisizofifishwa na zisizopungua asilimia 16 kwa Serikali.
Dk Kiruswa amefafanua kuwa, utaratibu wa ulipaji wa fidia kwa waguswa wa mradi unaendelea vizuri pindi utakapokamilika taratibu za kuanza ujenzi wa kiwanda cha uchataji wa madini ya niobium utaanza rasmi.
Sambamba na matumizi katika nyanja ya sayansi ya teknolojia pia madini ya Niobium hutumika katika mitambo ya uchorongaji katika utafiti na uchakataji wa mafuta, gesi pamoja na utengenezaji wa magari.