Tanzania, Msumbiji kukuza maendeleo, ustawi wa wananchi na uchumi

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Jamhuri ya Msumbiji katika kuleta maendeleo, ustawi wa wananchi na kukuza mshikamano barani Afrika.

Akihutubia katika Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Msumbiji zilizofanyika leo Juni 25 katika Uwanja wa Machava, jijini Maputo, Rais Samia amesema kuwa uhusiano wa Tanzania na Msumbiji sio wa kijiografia pekee, bali una mizizi ya kihistoria na mapambano ya pamoja dhidi ya ukoloni.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu kutoka Msumbuji imesema Rais Samia amekumbushia historia ya mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa Msumbiji kwa kuwapa hifadhi, licha ya kukabiliwa na changamoto za kiuchumi na matishio ya kiusalama kutoka kwa waliokuwa wakoloni wa Msumbiji.

Amewatambua waasisi wa mataifa haya mawili, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Samora Moisés Machel, kwa kuimarisha mshikamano wa kweli kati ya wananchi wa nchi hizi mbili wakati wa harakati hizo.

“Tulikuwa tayari kuchelewesha maendeleo yetu ili kuhakikisha ndoto ya ukombozi wa Msumbiji na mataifa mengine ya Kusini mwa Afrika inatimia,” amesema Rais Samia.

Vilevile, Rais Samia amepongeza jitihada za Msumbiji, baada ya kupata uhuru wake, katika kusaidia mataifa mengine ya Afrika kupata uhuru na kuishukuru Msumbiji kwa msaada uliotoa kwa Tanzania wakati wa Vita ya Kagera dhidi ya uvamizi wa Nduli Idi Amin, mwaka 1978-1979.

Halikadhalika, Rais Samia amepongeza hatua ya maendeleo iliyofikiwa na Jamhuri ya Msumbiji katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru wa nchi hiyo katika nyanja za elimu, afya na miundombinu, ambayo yaliletwa na dhamira ya kujenga jamii jumuishi na yenye matumaini.

Katika hatua ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara, Rais Samia ametangaza nia ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kuanzisha safari za moja kwa moja kati ya Tanzania na Msumbiji mwishoni mwa mwaka huu.

Rais Samia pia amewapongeza wananchi wa Msumbiji kwa kaulimbiu ya mwaka huu ya Mbio za Mwenge wa Umoja wa Kitaifa: “Miaka 50: Kuwainua Wanawake, Kujenga Usawa wa Kijinsia,” akisisitiza kuwa usawa wa kijinsia ni msingi wa mapinduzi ya kweli ya maendeleo.

Aidha, ametoa pongezi maalum kwa wanawake wapigania uhuru wa Msumbiji, akiwemo Josina Muthemba Machel na wengine kwa ujasiri usio na kifani.

Rais Samia amesema kuwa mchango wa wanawake katika harakati za ukombozi wa Msumbiji sio historia tu ya kupigiwa makofi, bali ni urithi wa kuenziwa na kizazi cha sasa kwa kuwawekea wanawake mazingira wezeshi ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Mapema leo, Rais  Samia alitembelea eneo la Kumbukumbu ya Mashujaa wa Nchi ya Msumbiji (Heroes’ Square) jijini Maputo, ambako aliweka shada la maua kama ishara ya heshima kwa mashujaa waliopoteza maisha yao wakipigania uhuru wa Msumbiji.

Rais Dkt. Samia atarejea nchini leo mara baada ya kukamilisha ziara yake ya kikazi Jamhuri ya Msumbiji.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button