DAR ES SALAAM: Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor amesema ushirikiano Kati ya Tanzania na Australia umechochea uboreshaji katika sekta mbalimbali kati ya nchi hizo mbili.
Amebainisha hayo wakati akimuaga Balozi wa Australia nchini, Luke Williams baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi leo jijini Dar es salaam.
Amesema Tanzania na Australia zimekuwa na uhusiano mzuri unaoendelea kuimarisha ushirikiano katika elimu, utalii, madini nishati, mabadiliko ya tabia nchi pamoja na biashara na uwekezaji.
Ameongeza kuwa ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Australia ni jambo lilochochewa na Balozi Williams wakati akitekeleza majukumu yake ya kibalozi.
“Katika kipindi chako umeiwakilisha vyema Australia na kuonesha mafanikio makubwa ambayo yamefikiwa kati ya Tanzania na Australia.
Kazi yako imechochea uboreshaji wa sekta za elimu, utalii, madini, nishati, uchumi wa buluu na kuchangia ukuaji wa sekta ya biashara uwekezaji katika nchi zetu, ni matumaini yangu kuwa utaendelea kuwa Balozi mwema kwa Tanzania nchini Australia na kokote uendako Duniani,” amesema Balozi Mbarouk.
Kwa upande wake Balozi Williams, ameeleza jinsi Serikali ya Tanzania ilivyo onesha ushirikiano wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake ya kibalozi.
“Kwa kweli ni ngumu sana kuaga lakini haya ndiyo maisha ya wanadiplomasia hakuna budi, siku zote nitakumbuka utu na ukarimu wa Watanzania,” amesema Williams