DAR ES SALAAM: SERIKALI ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Urusi wamesaini vipengele muhimu vya makubaliano ya mfumo unaolenga kuimarisha ushirikiano wa biashara na kiuchumi baina ya nchi hizo mbili.
Hafla ya utilianaji saini makubaliano hayo imefanyika leo jijini Dar es Salaam na kuhitimisha mkutano wa kwanza wa Tume ya Pamoja ya Biashara na Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili.
Tukio hilo la siku mbili lilijumuisha vikao kadhaa, vikiwemo mkutano wa wataalamu, shughuli kuu za tume ya pamoja, na kongamano la uwekezaji.
Majadiliano hayo yalihitimishwa na kikao cha ngazi ya juu cha mawaziri, ambapo mikataba hiyo ilisainiwa rasmi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo na Waziri wa Maendeleo ya Uchumi wa Urusi, Maxim Reshetnikov.
Katika taarifa ya pamoja, mawaziri hao walisisitiza ahadi ya nchi zao katika kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kiuchumi.
“Kwa miongo sita, Tanzania na Urusi zimedumisha uhusiano thabiti wa kisiasa na kiutamaduni, na hivyo kukuza maendeleo katika elimu, sayansi na teknolojia. Mikataba mipya inalenga kupanua ushirikiano huu katika sekta muhimu za kiuchumi, na kutengeneza fursa za ukuaji wa pande zote mbili,” amesema Prof. Mkumbo
Mfumo huo unahusisha maeneo kadhaa ya kimkakati, ikiwa ni pamoja na viwanda na biashara, fedha, nishati, kilimo, elimu, uchukuzi, afya, na teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).
Zaidi ya hayo, mawaziri walitambua maliasili, utalii, utamaduni na michezo kama sekta muhimu za ushirikiano chini ya ushirikiano huo mpya.
Kwa upande wake Waziri wa Uchumi na Maendeleo wa Shirikisho la Urusi, Maxim Reshetnikov alisifu maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania na kusisitiza umuhimu wa kuianzisha kama mshirika wa kimkakati barani Afrika.
“Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazokua kwa kasi kiuchumi katika kanda, na tumejitolea kukuza ushirikiano wa muda mrefu ili kufungua fursa mpya za biashara,” amesema Reshetnikov