TIMU ya taifa ya Kriketi kwa vijana chini ya miaka 19 imeanza vyema michuano ya Afrika daraja la pili kufuzu Kombe la Dunia la Baraza la Kimataifa la Kriketi (ICC) baada ya kuichapa Nigeria kwa mikimbio 128-127.
Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Gymkhana Dar es Salaam Tanzania imecheza wiketi nne na Nigeria 10.
Nahodha wa timu hiyo Laksh Bakrania amesema mchezo ulikuwa mzuri na mgumu ila juhudi zao zimewasaidia kupambana na kushinda.
Kesho Tanzania itakiwasha dhidi ya Ghana ambayo imeshinda mchezo dhidi ya Msumbiji kwa mikimbio 81-80.
SOMA: Mashindano ya kriketi kimataifa kuanza leo
Michuano hiyo ya Afrika iliyoanza leo inafanyika kwenye viwanja vya Gymkhana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo inashirikisha nchi nane ambazo ni Tanzania, Nigeria, Malawi, Msumbiji, Ghana, Botswana, Sierra Leone na Rwanda.
Tanzania ipo kundi B lenye timu za Nigeria, Msumbiji na Ghana huku kundi A kukiwa na Sierra Leone, Rwanda, Botswana na Malawi.
Mratibu wa mashindano hayo Atif Salum amesema nchi mbili kwa kila kundi zitaenda kucheza nusu fainali na zile zitakazofanya vizuri zitaenda fainali.
“Kutakuwa na mchezo pia wa kutafuta mshindi wa tatu. Timu tatu zitakazofanya vizuri zitafuzu daraja la kwanza,”amesema.
Mwenyekiti wa Chama cha Kriketi Tanzania (TCA) Dk Balakrishna Sreekumar amesema wanataka kuinua mchezo huo na kuhakikisha unakuwa miongoni mwa Michezo maarufu nchini huku akiishukuru serikali kwa kuwa pamoja nao.
Amesema wamealika vijana100 kutoka shule 10 za Dar es Salaam ili kutizama michezo huo na kuwapa hamasa ya kujiunga.
Michuano hiyo inatarajiwa kuendelea hadi Agosti 11 watakapopatikana washindi watatu watakaofuzu daraja la kwanza na kushiriki fainali za Dunia zitakazofanyika Sri Lanka 2026.