ADDIS ABABA: TANZANIA imetoa mwito kwa taasisi za fedha za kimataifa zitoe mikopo yenye riba nafuu ili nchi zinazokopa zikuze uchumi na kufikia malengo ya maendeleo endelevu.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Amina Khamis Shaaban amesema katika kikao cha kwanza cha Kamati ya Maandalizi ya Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Ugharamiaji kwa Maendeleo Endelevu (FfD4) kilichofanyika mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.
SOMA: Bajeti ya tril 49/- kuleta nafuu
Amina amesema katika kuhakikisha nchi zinaongeza rasilimali za ndani ni wakati sasa wa Umoja wa Mataifa (UN) kukamilisha mfumo wa ushirikiano wa kimataifa wa kodi ili kuzisaidia nchi kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya maendeleo.
“Tumesisitiza kuhusu upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hili ni jambo muhimu na kama tunavyojua sasa hivi tabianchi inaathiri nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania,” alisema
Alisisitiza pia vijana wapatiwe mikopo kwa ajili ya kufanyia biashara ili wajikwamue kiuchumi na kusaidia kuleta maendeleo ya nchi.