Tanzania yazindua rasmi ubalozi Algeria

Serikali ya Tanzania imezindua rasmi ubalozi wake jijini Algiers, Algeria.

 

Ufunguzi huo umefanywa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Stergomena Tax na kuhudhuriwa na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora wa Algeria, Ahmed Attaf,  Balozi wa kwanza wa Algeria kuhudumu nchini Tanzania,  Noureddine Djoudi na Jumuiya ya Wanadiplomasia nchini Algeria.

Kiwango cha ubadilishaji wa biashara kati ya Tanzania na Algeria ni cha chini ikilinganishwa na fursa nyingi zilizopo. Algeria yenye eneo lake la kimkakati na uchumi inatoa fursa kubwa kwa biashara za Tanzania. 

Akihutubia kwenye ufunguzi wa ubalozi huo Waziri Tax ameeleza kuwa Tanzania na Algeria zimejizatiti kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kwa lengo la kukuza ushirikiano wenye maslahi kupitia sekta za kipaumbele kama vile sekta za kilimo, madini, utalii, mafuta na gesi, vifaa tiba, viwanda, nishati pamoja uchumi wa buluu.

Naye  Attaf ameeleza kuwa ziara ya Waziri Tax imekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa wamepata fursa ya kuzungumza masuala ya ushirikiano katika sekta za biashara, uwekezaji na sekta nyingine muhimu kwa maendeleo ya mataifa hayo mawili.

“Balozi zinafaa kuendelea kuwa madaraja ya muhimu kati ya watu, nchi na mataifa.  Balozi zetu zinawajibika na kukuza, kuimarisha ushirikiano na uhusiano kati ya nchi na nchi ili kuleta tija zaidi na kuziwezesha nchi zetu kunufaika kiuchumi,’’ amesema Attaf.

Ufunguzi wa Ubalozi umefanyika pembezoni mwa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria, ambao umemalizika kwa mafanikio na kuwezesha kusainiwa kwa Hati 8 za Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta za nishati, mafuta na gesi, elimu na teknolojia, mafunzo ya diplomasia, kumbukumbu na nyaraka, ulinzi na usalama, ushirikiano wa kidiplomasia, kilimo na afya. 

Uhusiano kati ya Algeria na Tanzania uliasisiwa mwaka 1963 mara baada ya uhuru wa Tanganyika. Tangu wakati huo nchi hizi zimeendelea kushirikiana katika maeneo mbalimbali kwa maslahi ya pande zote. Vilevile katika kuimarisha ushirikiano huo Tanzania imefanya ufunguzi wa Ubalozi wake nchini Algeria ambao ulianza kutekeleza majukumu yake tangu mwaka 2017.

Viongozi wengine waliohudhuria ufunguzi huo ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, Naibu Makatibu Wakuu kutoka Wizara za Elimu, Sayansi na Teknolojia, Nishati na Mambo ya Ndani ya Nchi.

Habari Zifananazo

5 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button