Tanzania, Zambia zakubaliana kukuza ushirikiano, uhusiano

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania na Zambia zimekubaliana kuendelea kudumisha ushirikiano na uhusiano kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Kwa kuzingatia makubaliano hayo nchi hizo zimesaini makubaliano ya awali yanayogusa sekta za ulinzi, sayansi, teknolojia, ubunifu na utafiti na ujenzi wa bomba la gesi asilia.

Pia, Tanzania na Zambia zimesaini mikataba inayoshirikisha sekta ya umma na binafsi ya ushirikiano katika biashara na uwekezaji.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuzungumza na mwenyeji wake Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, Rais Samia alisema Tanzania na Zambia zipo tayari kuimarisha ushirikiano ulioasisiwa na waasisi wa mataifa hayo, Julius Nyerere na Kenneth Kaunda.

Alisema ziara yake Zambia imekuwa ya mafanikio kwa kuwa imewezesha kumaliza changamoto na vikwazo vilivyowakabili wafanyabiashara.

Rais Samia alitaja mafanikio hayo ni kusainiwa kwa makubaliano ya awali sita na mikataba miwili na kwamba katika siku za usoni yatasainiwa makubaliano na mikataba mingi zaidi.

Alisema hati za makubaliano zilizosainiwa zikiwemo za serikali na sekta binafsi itaongeza chachu ya kuharakisha maendeleo.

Rais Samia aliishukuru Serikali na watu wa Zambia kwa kumualika katika maadhimisho ya Miaka 59 ya Uhuru na akawashukuru Wazambia kwa ukarimu wao kwake na kwa ujumbe aliofuatana nao.

Rais Hichilema alimshukuru Rais Samia kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 59 ya uhuru wa nchi hiyo na kwa zawadi ya hekta 20 katika bandari kavu ya Kwala mkoani Pwani kwa ajili ya mizigo ya Zambia.

Alisema eneo hilo lazima litumike kusaidia kuimarisha zaidi biashara baina ya nchi hizo.

Aidha, Rais Hichilema aliomba Tanzania ishirikiane na Zambia pia katika sekta ya kilimo kwa kuwa wana fursa ya kuwa ghala la chakula kwa Afrika na kuchangia pia kuilisha dunia.

Alisema ziara hiyo imeimarisha miradi ya kimkakati inayotekelezwa kwa pamoja likiwemo Bomba la mafuta la Tanzania na Zambia (Tazama), reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) na miundombinu ya barabara ili kukuza uchumi.

Pia, Rais Hichilema aliagiza hati za makubaliano ya awali na mikataba vifanyiwe kazi ili viwe na manufaa kukuza uchumi.

Miongoni mwa hati hizo zilihusu masuala ya ulinzi na usalama na hati ya makubaliano kati ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) na Wakala wa Maendeleo Zambia.

Nyingine ni hati ya makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Jamhuri ya Zambia kuhusu mradi wa usafirishaji wa gesi asilia kutoka Tanzania na Zambia.

Pia imesainiwa hati ya makubaliano kati ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Wakala wa Maendeleo Zambia na hati ya makubaliano ya ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Jamhuri ya Zambia katika sayansi, teknolojia na ubunifu.

Pia, ulisainiwa mkataba wa utekelezaji kati ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jeshi la Ulinzi la Zambia kuhusu programu ya kubadilishana wanafunzi wa kozi ya ukamanda na unadhimu.

Pia ulisainiwa mkataba wa utekelezaji kati ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jeshi la Ulinzi la Zambia kuhusu programu ya kubadilishana wanafunzi wa kozi ya ofisa-Cadet.

Rais Samia na Rais Hichilema pia walishuhudia kusainiwa kwa mkataba wa utekelezaji kati ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jeshi la Ulinzi la Zambia kuhusu ushirikiano katika huduma za tiba.

Hichilema alieleza namna ushirikiano ulivyoleta faida kwa nchi hizo na akatoa mfano namna alivyoitumia reli ya Tazara kwenda Dar es Salaam wakati anafanya biashara ya magari.

 

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button