UHAWILISHAJI fedha unaofanywa na mpango wa kunusuru kaya masikini nchini (TASAF) unaelezwa kuwa kichocheo kikubwa kwa walengwa wa mpango wenye kipato duni kuboresha makazi yao na kujenga nyumba bora vijijini.
Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Wilaya Kasulu mkoani Kigoma, Maria Tarimo alisema kuwa katika vijiji 61 vinavyonufaika katika mpango huo, walengwa wake karibu robo tatu wamejenga nyumba bora, ukilinganisha na nyumba walizokuwa nazo kabla ya kuanza kupokea fedha kupitia mpango huo.
Tarimo alisema kuwa siri ya mafanikio ya utekelezaji huo na kuwezesha walengwa kuboresha makazi yao na kujenga nyumba bora inatokana na kuanzisha miradi midogo midogo ya kiuchumi na vikundi vya kukopeshana, ambapo wameweza kupata fedha na kuboresha makazi yao.
“Kwa sasa walengwa wengi wana hali nzuri hasa kwenye makazi bora na uanzishaji wa miradi ambayo imewasaidia kuwaongezea kipato tofauti na pesa wanayopokea na hiyo inatokana na elimu ya kusaidia jamii ambayo ni sehemu ya mpango huo, ambapo walengwa wengi wameweza kutekeleza na kuboresha maisha yao,”alisema Tarimo.
Walengwa wa mpango huo waliozungumza na timu ya waandishi wa habari waliokuwa wakitembelea kuona maendeleo ya utekelezaji wa mpango huo, akiwemo Feleciana Karima kutoka kijiji cha Nyamnyusi halmashauri ya Wilaya Kasulu, alisema kuwa ushiriki wake kwenye mpango wa uhawilishaji fedha TASAF umebadilisha maisha yake kwa kiasi kikubwa.
Karima alisema alifiwa na mume wake ambaye aliamuachia watoto sita wakiwa wanaishi katika nyumba ya udongo ya vyumba viwili na varanda iliyoezekwa kwa nyasi, lakini miaka mitano baadaye aliweza kubadilisha nyumba hiyo kuwa ya matofali ya kuchoma na kuezekwa kwa bati.
Kama hiyo haitoshi alisema kuwa aliongeza nyumba nyingine ya vyumba viwili na varanda ya matofali ya kuchomwa na kuezekwa kwa bati, sambamba na kujenga choo bora tofauti na choo cha matundu.
Kwa upande wake mnufaika mwingine wa Mpango huo, Fellister Gerrald ambaye alifiwa na mume wake na kumuacha na watoto watano alisema kuwa baada ya kifo cha mume wake hali ilikuwa ngumu sana, lakini baada ya kuingizwa kwenye mpango wa TASAF maisha yake yamebadilika sana.
Mnufaika huyo alisema kuwa aliweza kujenga nyumba baada ya kuanzishwa miradi ya ujasiliamali ikiwemo kununua vifaranga 48, ambavyo vilikua na akauza kuku 39 ambao aliweza kuanza kubadilisha makazi yake na kujenga nyumba ya tofali za kuchomwa na kuezekwa kwa bati.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kasangezi Halmashauri ya Wilaya Kasulu, Harun Banyegeko amewathibitishia waandishi wa habari kuwepo kwa mabadiliko makubwa kwa walengwa wa TASAF, ambo wameweza kuboresha makazi yao na kujenga nyumba bora jambo ambalo anasema limefanywa kwenye vijiji vingi mkoani Kigoma kupitia walengwa wa mpango huo.