TBS kuendelea kutoa elimu uthibitishaji ubora wa bidhaa

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limesisitiza kuendelea kutoa elimu kwa wazalishaji wa bidhaa mbalimbali ili kuhakikisha wanathibitisha ubora wa bidhaa zao.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Ofisa Masoko wa TBS, Rhoda Mayungu, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na ushiriki wa shirika hilo kwenye Maonesho ya 50 ya Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu yaliyofanyika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.

“Tumeshiriki maonesho haya ili kutoa elimu kwa wananchi juu ya huduma tunazozitoa na kuwapa hamasa ya kufika katika banda letu kujua majukumu yanayotekelezwa na TBS,” alisema.

Alitoa wito kwa wanaozalisha bidhaa nchini hasa wajasiriamali wadogo na wa kati kuhakikisha wanathibitisha ubora wa bidhaa zao ili kupata masoko ya uhakika.

Hata hivyo, alisema ili wajasiriamali waweze kupata huduma hiyo bure inayotolewa na serikali kupitia TBS ni lazima awe na barua ya utambulisho kutoka Sido.

“Wakishakuwa na barua ya utambulisho kutoka Sido wakija kwetu tunathibitisha bidhaa zao bure,” alisema.

Aidha, alisema kupitia maonesho hayo walitoa elimu juu ya mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2019 ambapo baadhi ya majukumu yaliyokuwa yanatekelezwa na iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) yalihamishiwa TBS.

Alisema kupitia mabadiliko hayo kwa sasa majukumu ya usajili wa bidhaa ya chakula na vipodozi zinafanyika TBS.

Aliwataka wananchi wasinunue bidhaa iliyokwisha muda wake wa matumizi ikiwa ni pamoja na kuepuka ulaghai wa wauzaji wa bidhaa hizo.

Alifafanua kwamba baadhi ya wenye maduka wamekuwa walaghai kwa kuwaambia wananchi kwamba licha ya bidhaa husika kuisha muda wake wa matumizi, lakini inaweza kutumika miezi mitatu mbele.

Habari Zifananazo

Back to top button