KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili jumla ya miradi 526 yenye thamani ya takribani Dola bilioni 5.7 kwa kipindi cha mwezi Januari 2023 hadi Januari 2024.
Akizungumza mkoani Mtwara wakati wa semina ya siku moja iliyohusisha wawakilishi wa wafanyabiashara wa mkoa huo na kituo hicho cha uwekezaji, Meneja Uhamasishaji Uwekezaji wa ndani kutoka TIC Felix John amesema matarajio yao ni kutengeneza ajira 230,000 endapo miradi hiyo itakamilika.
Amesema asilimia 45 inamilikiwa na kutekelezwa na watanzania, asilimia 28 inatekelezwa na wageni na asilimia 27 inatekelezwa kwa ubia baina ya watanzania hao na wageni.
Aidha amewataka watanzania kuwekeza katika miradi mbalimbali kwani kumekuwa na faida nyingi ikiwemo uwekezaji wa uhakika.
Pia kujenga uzalendo, kutekeleza kwa vitendo dhana ya ushirikishwaji kwa kuwashirikisha watanzania katika uchumi wao badala ya kuwaacha na kubaki watazamaji.
‘’Tuwekeza katika miradi mbalimbali kwani kumekuwa na faida nyingi ikiwemo uwekezaji wa uhakika, kujenga uzalendo”
“Swala lingine ni kutekeleza kwa vitendo dhana ya ushirikishwaji kwa kuwashirikisha watanzania katika uchumi wao badala ya kuwaacha na kubaki watazamaji’’amesema John.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara Abdallah Mfinanga ameushukuru uongozi wa TIC kwa kuendelea kutoa elimu juu ya uwekezaji wa ndani na kuwataka wafanyabiashara mkoani humo kuchangamkia fursa hizo.
Mwekezaji mdogo mkoani humo, Mwajuma Ankoni ameishukuru TIC na serikali kwa ujumla kwa kutoa elimu hiyo ya uwekezaji kwa wafanyabiashara wa mkoa huo.
Amesema hapo awali walikuwa na tafsiri ya kuwa uwekezaji huo unahusisha watu wenye mitaji mikubwa na makampuni kutoka nje ya nchi.
‘’Mimi kama mwekezaji mdogo nimekuwa nikikutana na changamoto mbalimbali ikiwemo kupoteza mitaji inayosababisha na kushuka kwa soko la bidhaa tunazozalisha”
Amesema wakati mwingine inasababishwa na kutokuwa na soko la uhakika hivyo kupitia elimu hiyo ni matumaini yake itakuwa ni moja ya fursa kwao kupitia uwekezaji huo.